Aliyekuwa mgombea wa urais
kupitia Chadema na Ukawa, Edward Lowassa amesema ataendelea kushiriki
kikamilifu katika siasa na kubainisha kuwa utaendeleza mapambano ya
mabadiliko kwa kudai Katiba Mpya.
Lowassa aliwaambia
wanahabari leo kuwa kasi ya ufanyaji wa siasa itaongezeka kuliko
ilivyokuwa awali na kwamba kwa sasa anaweza akawa “amepoteza pambano
lakini siyo vita.”
Kauli hiyo ya Lowassa inabadilisha
msimamo wake wa awali aliokuwa wameutangaza kupitia mahojiano na Shirila
la Habari la Uingereza (BBC) kuwa iwapo angeshindwa kinyang’anyiro
hicho cha urais angeenda kuchunga ng’ombe kijijini kwake Monduli mkoani
Arusha.
Mwanasiasa huyo, ambaye pia ni waziri mkuu wa
zamani, alisema Ukawa itaendelea kudai Katiba Mpya ya wananchi
itakayohakikisha kuwa Tanzania inakuwa na tume huru ya uchaguzi na
serikali inayowajibika kwa umma.
“Ni wazi kuwa uchaguzi
mwingine katika mazingira ya sasa na chini ya katiba ya sasa hauwezi
kuzaa matunda tofauti. Bila katiba mpya ya wananchi, Tanzania haitakuwa
na demokrasia na itaendelea kuwa nchi inayotawaliwa kwa mizengwe na
udikteta wa CCM,” alisema Lowassa.
Maoni
Chapisha Maoni