MAGUFULI ATUA DODOMA NA JINA LA WAZIRI MKUU,ASAFIRI KWA BASI


RAIS John Magufuli amewasili mkoani Dodoma kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuongoza Tanzania akiwa ametumia njia ya barabara huku akiwa na siri moyoni ya nani atakuwa Waziri Mkuu wake. Njia aliyotumia kufika Dodoma imewashangaza wengi kutokana na ukweli kwamba marais waliotangulia wamekuwa wakitumia usafiri wa ndege.
Baada ya kuwasili Ikulu Ndogo ya Rais iliyopo Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma akitokea jijini Dar es Salaam, alipokewa na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Chamwino Ikulu, Joseph Seganje, wananchi wamefarijika kuona Rais huyo akiishi kwenye Ikulu hiyo kama alivyokuwa ameahidi. “Tayari tumempokea Rais wetu na wananchi wana furaha isiyo na kifani,” alisema Seganje.
Wakizungumza mapema wiki iliyopita, baadhi ya wakazi wa Chamwino Ikulu walisema itakuwa ni faraja kubwa kwa Rais kuishi kijijini hapo. Alice Chidong’oi alisema Dk Magufuli ni kiongozi anayeonesha nia ya dhati ya kuwatumikia watu wake kwa kujali zaidi wanyonge kama ilivyokuwa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Tunaamini akiishi hapa atakuwa sehemu ya jamii ya Wana Chamwino na hilo litasaidia hata kuboreshwa kwa huduma za jamii ikiwemo maji,” alisema Chidong’oi. Alisema hiyo itakuwa fursa nzuri kwa wakazi wa eneo hilo kufanya biashara, kwani uwepo wake ndani ya wilaya hiyo utaongeza idadi ya wageni.
Mkazi mwingine, Stanley Richard, alisema vijana wa Chamwino wanapenda kazi na Dk Magufuli akiwa hapo itakuwa ni kazi tu. “Ni mtu ambaye anapenda kazi na sisi vijana tunapenda kufanya kazi, tutampa ushirikiano mkubwa katika kipindi chote atakachokuwa madarakani,” alisema.
Alisema alifurahi alipochaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani alijua nchi imepata kiongozi ambaye yuko tayari kuwaletea wananchi wake mabadiliko. Tayari Serikali mkoani hapa imepiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya hadhara na maandamano wakati wa vikao vya Bunge vikiendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa, alisema amri hiyo ya kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa bado inaendelea ili kuweka utulivu muda wote wa vikao vya Bunge.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Bunge, kesho Alhamisi, Bunge litapokea na kuthibitisha kwa kupiga kura jina la Waziri Mkuu wa 11 wa Tanzania ambalo Dk Magufuli atakuwa ameliwasilisha kwa Spika Job Ndugai.
Kwa hiyo, Dk Magufuli atakuwa ametua mjini hapa akiwa na siri yake moyoni ya nani atakuwa Waziri Mkuu wake kwa miaka ya mwanzo ya utawala wake inayokoma mwaka 2020.
Mbali ya kutoa jina la Waziri Mkuu, Dk Magufuli anatarajia kulihutubia Bunge, Ijumaa alasiri baada ya kuwa amemwapisha Waziri Mkuu asubuhi. Hotuba yake itakuwa dira ya utawala wake kwa miaka mitano ijayo.

Maoni