MAJJID-MITA 200 ZA UKAWA ZITAMPITISHA DR TULIA KUWA SPIKA??


Ndugu zangu,
Jioni ya leo zimetufikia habari kuwa kati ya majina 21, Kamati Kuu CCM imepitisha matatu; Job Ndugai , Abdul Ali Mwinyi na Dr Tulia Ackson Mwansasu. Tunaohangaika na kuchambua mambo ya siasa kuna ishara tunaziona, zilianzia na ndugu Masaburi kutoa jina dakika za mwisho.
Na siasa ni mchezo ambao mara nyingi, kama ilivyo soka, unaweza kuamuliwa katika dakika za lala salama.
Yumkini katika majina matatu yaliyorudishwa kuna mbili turufu na moja jokeli.
Kuna wanaoweza kunishangaa, nikisema kuwa jokeli hapa aweza kuwa yule ambaye wengi wanamdhania, lakini siye.
Spika wa bunge la 11 atakuwa spika wa Bunge jipya lenye vijana wengi na litakalosisimka. Katika hili naiona nyota ya Dr Tulia ikiwa ang'avu zaidi na iliyopaishwa zaidi siku mbili kabla ya uchaguzi mkuu uliopita.
Ni pale, kama nilivyopata kuandika nyuma, Ukawa walipofanya kosa kubwa la kiufundi kwa kupitia mgombea wao viti maalim, Ammy Kibatala, kufungua madai mahakama kuu kupinga sheria ile ya mita 200.
Dr. Tulia Ackson Mwansasu, akiwa kama Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akawa amepigiwa penalti mikononi. Yeye na mawakili wa Serikali walizipangua hoja za Ukawa na kushinda. Kesi ile maarufu na hukumu yake, kiukweli ilichangia kwa kiasi kikubwa anguko la ukawa. Maana, viongozi wakuu wa ukawa walitamka hadharani, kuwa ushindi ni kusimama mita 200, tafsiri yake, marufuku ya mahakama ya mita 200 ni kuwa hakuna ushindi. Kuna wapiga kura wa UKAWA ambao hawakuona hata maana ya kuwapigia kura UKAWA au kwenda kabisa kupiga kura.
Job Ndugai anafahamika na mwenye uzoefu, lakini, kuwepo kwake muda mrefu na hata kushiriki minyukano ya kimakundi iliyopelekea, hata wakati fulani wa Bunge la Katiba, Ndugai kutokuwepo kwa muda mrefu kwa ' majukumu' mengine kunampungizia nafasi ya kupitishwa kuongoza bunge jipya lenye kuhitaji msisimko mpya.
Abdul Ali Mwinyi pamoja na kuwa ni Mbunge wa Afrika Mashariki na mtoto wa Rais Mstaafu, bado linabaki kuwa ni jina geni katika muktadha niliouelezea hapo juu.
Yote kwa yote, katika hali halisi Spika wa Bunge la 11 atatoka CCM, na katika watatu waliotajwa leo, bado naliona jina la Dr Tulia Ackson Mwansasu likiwa na nafasi kubwa...
Maggid.

Maoni