Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Makala: Buriani Komredi Mawazo, Mpe Hongera Zangu Ken Saro-Wiwa


Salamu pia kwa Patrick Balisidya – kweli wema hawana maisha

Dhamira yangu ni thabiti mno, utayari wangu kutimiza azma ya mioyo ya Watanzania na ile ya chama changu haipimiki. Hakuna gharama itakayokuwa ngumu kwangu kuilipa kwa ajili ya ukombozi wa taifa langu, ninamaanisha HAKUNA…..Nitajie gharama yoyote nitakuambia I’m ready to pay (nipo tayari kuilipa) ili mradi niwe na uhakika ya kwamba kama ni damu yangu itakuwa haimwagiki bure kwa faida ya wachache” –Alphonce Mawazo.
Hii ni kauli yako ya kijasiri katika kusimamia kile ulichoamini, uliyoitoa kwetu marafiki zako kupitia ukurasa wako wa Facebook Februari 26, 2014.

Jumamosi ya Novemba 14, 2015 nikiwa ofisini na baadhi ya watendaji wenzangu tulipata taarifa kuwa Alphonce Mawazo umeshambuliwa na hali yako ni mbaya. Tulishtuka sana na kuanza kufanya mawasiliano na viongozi waliopo Geita ili jitihada zifanyike kuokoa roho yako kamanda wetu.
Nilikumbuka ni jana yake tu niliongea nawe kuhusu safari yetu ya Dodoma na kuahidiana kubadilishana vitabu. Nilikuahidi kitabu “Facing Dictators(kuwakabili maimla)’’ kilichoandikwa na Anthony Eden na kingine “Profiles in Courage” kilichoandikwa na John F.Kennedy aliyekuja kuwa Rais wa baadaye wa Marekani.

Muda mfupi baadaye nikapokea simu kwamba Alphonce Mawazo ameaga dunia. Sikuamini, nilitaharuki.
Kwamba sasa siasa zetu zimefikia hatua kwamba ukiwa mpinzani ni kujichagulia adhabu ya kifo? Kwamba rafiki yangu na mwanamageuzi Alphonce Mawazo umedhulumiwa nafsi yako kwa sababu tu ya tofauti yako kiitikadi, kwa sababu tu unatumia haki yako ya kikatiba kujichagulia mrengo wa kisiasa? Ulichostahili kama matunda ya demokrasia ya mfumo wa vyama vingi ni kucharangwa mapanga na kushambuliwa kwa visu, marungu na silaha nyingine za jadi kama vile ni mhalifu hadi kupoteza pumzi yako ya mwisho? Kweli?

Ninajiuliza ni kwa nini basi tuliridhia mfumo wa vyama vingi ikiwa hatuwezi kuvumilia watu wenye misimamo na hoja kinzani? Chembechembe hizi za uhafidhina zilizopaliliwa na mfumo wetu wa utawala tangu chama tawala kiliposhika hatamu ndizo zilizozalisha ujasiri huu wa kishetani. Ujasiri wa kumwaga damu kwa wanaharakati na wapinzani dhidi ya chama tawala. Woga (cowardice) wa kuvumilia na kujibu hoja kinzani kwa hoja.
Mawazo umekufa kifo cha kikatili, umekufa ukitetea na kulinda imani yako uliyoisimamia. Ningekuwa na uwezo wa kulaani, ningemlaani yeyote aliyehusika katika kupanga na kutekeleza uharamia huu.

Hakuna itikadi yoyote ya kisiasa inayoweza kuhalalisha umwagaji wa damu. Ni itikadi ya shetani na sera zake pekee inayoweza kuhalalisha kwa kiwango chochote ufedhuli huu. Itikadi hizi ndizo zilizoongoza sera za mauaji ya wanaharakati na watetezi wa haki ulimwenguni kama akina Steve Biko kule Afrika Kusini, mtetezi na mpigania haki za weusi Martin Luther Jr kule Marekani, Ken Saro-Wiwa kule Nigeria na wengineo.
Kwenye imani zetu za dini waathiriwa wa itikadi hizi za kishetani na fitna zake ziliwakumba wale waliokuwa na msimamo thabiti wa kuhubiri na kusimamia imani zao katika utetezi wa haki.

Katika Uislamu wapo mashahidi waliofia imani yao katika kueneza uislamu kama Swahiba wa Mtume ‘Umar bin Al-Khattwaab aliyeuawa na Abu Lu-u lu-u ambaye alikuwa mtumwa wa Al-Mughiyrah bin Sh’bah alikuwa mateka wa vita. Alikwenda kwa ‘Umar kulalamikia juu ya kodi kubwa hivyo, alimwambia: “Unacholipa si kikubwa.”

Aliondoka na ‘Umar kisha alichukua jambia lenye ncha tatu na kulificha mpaka alfajiri ambapo ‘Umar angeamsha watu kwa ajili ya Swalah ya Subhi, na alimchoma mara tatu. Pigo moja lilikuwa chini ya kitovu ndilo lilosababisha kifo.
Katika Ukristu wapo mashahidi waliofia imani ya kikristo kama Mtume Paulo. Aliuawa nje ya kuta za Roma kwa kukatwa kichwa wakati wa dhuluma za mfalme Nero kati ya mwaka 64 na 67 Baada ya Kristu.

Juu ya kaburi lake lilijengwa kanisa kubwa ambalo liliteketea kwa moto katika karne ya 18 likajengwa upya na hadi leo linapokea hija za Wakristo wengi, hasa katika "Jubilei ya Mtume Paulo" iliyotangazwa na Wakatoliki na Waorthodoksi kwa mwaka 2008/2009.

Mawazo ulikuwa ni mwanasiasa wa kipekee na mwanamapinduzi uliyekuwa na msimamo thabiti juu ya kile ulichoamini. Kamwe katika kuwapigania Watanzania, na pia wakati huo huo kufikia ndoto zako hakuwahi kufungwa na itikadi za vyama. Utetezi wako wa haki na kupinga dhuluma dhidi ya Watanzania haukuwahi kukwazwa na kabila, itikadi za kidini wala kisiasa. Historia yako kisiasa ndio ushuhuda wa maisha yako.

Mengi yameandikwa kuhusu harakati zako. Mengi yameandikwa kuhusu uaminifu, uchapakazi na unyenyekevu wako, si nia yangu kuongeza au kupunguza yaliyokwisha kusemwa. Huyu ndiye Alphonce Mawazo ninayemfahamu. Mwaka 2005 alijiunga na Chama Cha TLP ambapo hadi kufikia wakati huo, alikuwa Mwalimu wa Shule ya Sekondari Bondeni jijini Arusha, akifundisha masomo ya Hisabati na Kiingereza.

Mwaka huo huo aligombea udiwani katika Kata ya Sombetini (TLP) na kushinda nafasi hiyo ya udiwani na baadaye mwaka 2007, alijiuzulu katika nafasi hiyo na kujiunga Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hivyo kuifanya kata hiyo kutokuwa na mwakilishi (diwani) kwa muda wa miezi michache.
Hadi kufikia mwaka 2008, Halmashauri ya Arusha kwa kipindi hicho (sasa Jiji la Arusha), ilitangaza kufanya uchaguzi mdogo na kati ya watangaza nia alikuwemo marehemu, Alphones Mawazo, aliyegombea kwa tiketi ya CCM na alichaguliwa na wananchi kushika nafasi hiyo kwa mara nyingine hadi 2010 ambapo ulifanyika Uchaguzi Mkuu katika nafasi za udiwani, ubunge na urais ambapo marehemu alishinda tena nafasi hiyo baada ya kugombea kwa tiketi ya CCM.

Mwaka 2012 akiwa mwanachama wa CCM na diwani wa kata hiyo, alijiuzulu nafasi yake na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lakini hakushiriki tena kutetea nafasi hiyo ya udiwani na badala yake aliongeza nguvu ya kutumikia na kukijenga zaidi Chadema katika mikoa wa Kanda ya Ziwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Kata ya Sombetini ilikaa kwa zaidi ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchelewa kutangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa kata hiyo hadi mwaka 2013 alipochaguliwa Ally Bananga kuwa diwani wa kata hiyo. Uchaguzi huo ulifanyika baada ya kuahirishwa na tume kutokana na mauaji yaliyotokea Juni 15, 2013 baada ya wafuasi na viongozi wa Chadema kushambuliwa kwa mabomu na risasi wakiwa katika mkutano wa hadhara.

Mwaka 2014, Alphonce Mawazo, achaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita ambapo alitumia muda mwingi na rasilimali zake pale ilipohitajika kufanya hivyo, kuzunguka maeneo mbalimbali ya taifa ili kuwapa elimu ya uraia hususani watu wa vijijini kwa kutumia usafiri wa aina mbalimbali, ikiwamo baiskeli.

Mwaka 2013, Mawazo alitoa gari lake akiwa Arusha na kuomba ‘speaker’ na mafuta ya kumfikisha Kanda ya Ziwa hasa vijijini ambako alisema ataenda kufia huko. Alisema yupo tayari kufa kutetea haki na kuhakikisha Watanzania wanyonge ambao watawala wanawatumia kama ngazi kujipatia madaraka na kuyatumia kifisadi.

Mimi binafsi nilikutana naye kwa mara ya kwanza Aprili 20, 2012, siku ya Ijumaa mjini Geita. Naikumbuka sana siku hii kwa sababu ilikuwa ni siku ya kihistoria katika kitabu changu cha kumbukumbu zangu kisiasa (Political Diary).

Ni mojawapo ya siku niliyonusurika kuvuliwa uanachama wa chama changu kutokana na misukosuko tunayokumbana nayo katika safari yetu kisiasa. Siku hiyo baada ya kikao cha ndani kilichoongozwa na viongozi wetu kitaifa, tulienda kwenye mkutano wa hadhara Uwanja wa Magereza mjini Geita.

Alphonce Mawazo alitoa hotuba kali na yenye kutia uchungu sana juu ya unyonyaji na unyama uliokuwa ukifanywa na kampuni zinazochimba dhahabu Geita zikilindwa na watawala wetu. Mita chache kutoka eneo la mkutano kulikuwa na kambi kubwa ya wakimbizi (Ndio, wakimbizi wa ndani) ambao ni Watanzania wenzetu walioporwa maeneo yao bila fidia na kampuni zinazochimba dhahabu na hivyo kukosa makazi.

Baaada ya mkutano ule nilikutana na Mawazo na kujadiliana naye kwa kina kuhusiana na ule unyama waliofanyiwa wananchi wa Geita. Sote tulikubaliana kuwa unyama ule haukuwa na tofauti na unyama uliokuwa ukifanywa na kampuni za kibeberu za kuchimba mafuta kule Niger Delta nchini Nigeria, enzi za utawala wa Dikteta Sani Abacha ambako kampuni zilizalisha mafuta na kutumia kemikali zenye sumu zilizoathiri afya za wananchi huku wananchi hao wakiishi maisha ya umasikini uliopindukia huku watawala wakilinda kwa nguvu ya dola kampuni hizo husika dhidi ya wananchi wao baada ya kunufaika kifisadi kutokana na mikataba ya ovyo ya uchimbaji mafuta.

Ni kwa sababu ya kupigania haki na kupinga dhuluma hii, mwanaharakati na mwandishi wa vitabu, Kenule Beeson Saro wiwa maarufu kama Ken Saro-Wiwa, aliuawa kwa kunyongwa na utawala wa kijeshi wa Dikteta Sani Abacha, Novemba 10,1995 akiwa na miaka 54.

Miaka 20 na siku 4 tu baada ya kuuawa mwanaharakati na mtetezi wa Niger Delta ya Nigeria, Novemba 14, 2015 historia ya Niger Delta ya Nigeria imefufukia Geita Tanzania. Alphonce Mawazo katika umri wa miaka 39 tu ameuawa akiwa na kiu ya kukamilisha ndoto zake.

Bado alikuwa katika mkakati wa kujiunga kuendelea na masomo yake hadi ngazi ya shahada ya uzamili (masters degree). Ni yeye aliyenitia moyo wa kuendelea na masomo yangu ngazi ya Ph.D.

Sote tuliamini katika misingi ya kujiandaa kiuongozi. Tuliamini kiongozi mzuri ni yule anayejiandaa au anayeandaliwa na pia anayetengeneza viongozi wengine wapya (succession plan). Tuliamini kila zama ina kitabu chake, kila zama na changamoto zake na kila zama na mitume yake. Tuliamini kulingana na umri wetu miaka 10 -20 ijayo itakuwa zamu yetu kushika usukani wa uongozi na kuiweka vyema ramani na dira ya siasa za nchi (political landscape) kwa mapenzi yake Mola.

Ni misingi hiyo iliyozidi kutuweka karibu na kukuza urafiki wetu na kupanga mipango ya baadaye katika harakati zetu kisiasa. Tulitambua kuwa taifa letu limejikuta katika matatizo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa na kushindwa kupata suluhisho kutokana na kutopata viongozi bora wenye uchungu na maendeleo, uzalendo na dira sahihi ya kuweza kuliinua taifa juu katika ramani ya dunia miongoni mwa mataifa mengine.

Tulidhamiria, kama ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu basi tunaweza kutoa mchango wetu katika kuujenga upinzani imara na kupambana na mfumo uliopo ili tuweze kuleta mageuzi kwa kuanzia na mapambano ya kifikra. Ni katika mtazamo huu tuliamua kutoa elimu ya uraia na kutiana moyo kila mtu kwa nafasi yake tukiamini kufanya hivyo pia ndoto zetu katika safari ya kisiasa zitatimia.

Septemba 2014 tulichukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama chetu ya kuwa wajumbe wa kamati kuu ya chama. Lengo likiwa ni kuendelea kutumia fursa hiyo kukomaza demokrasia ndani ya chama chetu na upinzani kwa ujumla. Hatukufanikiwa kwa sababu za kisiasa.

Mara nyingi Mawazo amekuwa akinikumbusha na kunitahadharisha kuwa makini katika harakati zetu hizi kupitia maneno ya Frank Underwood kwamba; “Njia ya kusaka ama kuelekea kwenye madaraka imepambwa/ imesakafiwa kwa unafiki na majeruhi”

Tuliendelea kupeana moyo na kujikita katika kukiandaa chama chetu kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu na pia sisi wenyewe tukijiandaa kuingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huo. Yeye aligombea Jimbo la Busanda nami nilijielekeza Jimbo la Rombo. Mauti yamemkuta akiwa katika mchakato wa kupinga mahakamani matokeo ya ubunge Jimbo la Busanda, yaliyompa ushindi mgombea wa CCM, Lolesia Bukwimba aliyetangazwa kupata kura 63,043 dhidi ya kura 45,019 alizotangazwa kupata yeye. Alphonce Mawazo alikuwa akichukia dhuluma, hakutaka kuonewa hata kidogo. Alianza mchakato wa kisheria kupinga matokeo hayo mahakamani kwa ushahidi wakati huo huo tukiendelea kujipanga zaidi kisiasa.

Kwa hakika, kama tulivyowatangazia Watanzania na dunia juzi kupitia vyombo vya habari, kila aliyehusika na mauaji haya tutahakikisha analipa kadiri ya uovu huu. Sisi marafiki na makamanda wenzako tutaipigania haki yako hadi tone la mwisho.

Tumekwishatoa wito kwa Jeshi la Polisi liwasake wote waliohusika la sivyo hiyo kazi tutaifanya sisi wenyewe. Hatutavumilia kuona damu yako isiyo na hatia ikimwagwa na watu wasiokuwa na utu, watu waoga ambao siasa zimewacheza vibaya. Hatutavumilia kuona haki yako ikikanyagwa hata kidogo. Tunaambiwa hata Jeshi la Polisi linazuia makamanda wenzako wasikuage kwa heshima zote. Tutaidai mahakamani na kuilinda haki yako hii.
Binti yako mdogo Precious amebaki bila baba, mkeo mpendwa Nuru amempoteza mume, Chadema na Ukawa wamempoteza kiongozi mahiri na taifa limemkosa kiongozi mwanamapinduzi na pengine Rais wa baadaye.

Mimi Binafsi nimekupoteza rafiki na Mshirika wangu katika safari ya kisiasa.Vitabu vyako nimpe nani sasa jembe langu? Umeniachia vitabu hivi nisome na nani sasa? Ndoto na mipango yetu ya kisiasa ya baadaye nitatekeleza na nani?

Mkoa wako wa Geita umemuachia nani? Nani wa kuwasemea wananchi wako wa Busanda? Tangulia rafiki mshirika wangu, nakuahidi katika kusimamia haki na kupinga dhuluma sitafungwa na itikadi za vyama, dini wala makabila.

Tafadhadhali tufikishie ujumbe kwa Mohammed Mtoi, mwambie kiti chake ofisini hakijapata mrithi bado. Waambie washirika wangu Faith Makundi na Allan Patrick, bado naishi ndoto yangu.

Ile safari yetu ya kwenda kwenye mapambano ya ukombozi Rombo iliyoishia pale Kibaha na wao kutangulia mbele za haki bado ipo. Ndoto ile inaishi bado. Waambie nawakosa sana na kadiri inavyokaribia Desemba 10, majonzi huzidi kuujaza moyo wangu.

Tufikishie salamu kwa Dk. Sengodo Mvungi, mwambie baadhi yao wale aliokuwa nao kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba sasa hivi wameungana na walionyonga maoni ya wananchi.

Mwambie Dk. Makaidi, bado uchaguzi wa urais wa Muungano umeonekana halali lakini wa Zanzibar alikopata kura nyingi Maalim Seif ukaonekana haramu. Utakapokutana na Wazanzibari waliouawa 2001 kule Pemba, waambie wafute machozi, hivi karibuni Wazanzibari watapata haki yao.
Utakapokutana na mwanaharakati Martin Luther Jr, mwambie Wamarekani weusi walipata haki zao na kiu na matamanio yake katika hotuba yake “I have a dream” imetimia, ungana naye kuiombea Tanzania ili kiu yako ya kutaka kuona Tanzania inaondokana na ubaguzi uliopo kati ya masikini na tajiri unaondoka.

Mpongeze Ken Saro-Wiwa kwa kuchochea harakati zetu katika mapambano. Mueleze jinsi alivyochochea kiu yako ya kupigania watu wa Geita kama alivyofanya yeye kule Niger Delta. Muhakikishie kwamba kile kitabu chako ulichoanza kuandika, kitamalizika ili fikra na maono yako yawe mojawapo ya nguzo muhimu katika kuijenga Tanzania mpya yenye haki na usawa. Mwambie kule Nigeria sasa utawala wa kiraia umerejea, demokrasia imekalia kiti cha enzi na sasa imekuwa mfano wa demokrasia zinazoendelea kukomaa kwa kasi barani Afrika.

Fikisha salamu zetu kwa Mwalimu Nyerere, mwambie mfumo wa vyama vingi aliourudisha haukupokelewa vyema na wenzake, mwambie kwamba wale wahafidhina hawawezi kuvumilia siasa kinzani. Mwambie taifa limejaa madoa ya damu za wanaharakati na wapinzani.

Ukikutana na mwimbaji (hayati) Patrick Balisidiya, mwambie huku duniani mashairi ya wimbo wake”Wema hawana maisha” aliotuachia unatuzidishia simanzi na uchungu kipindi hiki tunapoomboleza kifo chako.

“Ni mashaka na hangaiko
Fitna chuki na wivu, dunia imepambika!
Yamejaa machukivu, hayapendezi hakika!
Wema wamepakwa jivu, hawataonekanika!
Ni mashaka yangalipo, wema hawana maisha...”

Haya tangulia komredi wangu, siku atakayopanga Mola wetu tutaonana. Tuombee huko uliko. Mwenyezi Mungu hatutakuhoji, kwamba ni kwa nini umeruhusu haya. Tutaendelea kukuabudia Mola wetu. Lala salama kamanda wetu, umemaliza mbio kishujaa!

Mwandishi wa makala haya Na Ben Saanane anapatikana 0768078523

Maoni