MREMA AILILIA TUME AMTAKA MAGUFULI KUMKUMBUKA KWENYE UONGOZI WAKE



Mwenyekiti wa Taifa wa TLP na aliyekuwa Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana kuhusu mchakato wa uchaguzi ulivyofanyika jimboni humo uliofanya kushindwa kutetea jimbo lake. Kulia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Nancy Mrikaria, aliyekuwa mgombea urais kwa chama hicho, Macmillan Lyimo (kulia kwa Mrema) na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Tiganya Vincent. (Picha na Fadhili Akida).

ALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Vunjo na Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema amempongeza Rais Mteule, Dk John Magufuli kwa kushinda urais na kumuomba katika uongozi wake amfikirie.
Aidha, mwanasiasa huyo, amelia na kile alichodai ni kuhujumiwa jimboni kwake Vunjo na hivyo kushindwa katika uchaguzi wa ubunge. Aliyeshinda ni James Mbatia wa NCCR- Mageuzi. Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi mkuu ambao alishindwa kutetea kiti chake cha ubunge jimboni Vunjo.
“Naomba Dk Magufuli atimize ahadi yake aliyoitoa baada ya kuja kwenye kampeni Vunjo na kusema, endapo sitapata ubunge, atanifikiria kwa kuwa anatambua utendaji kazi wangu,” alisema. Mrema alisema Dk Magufuli alipokwenda jimboni kwake, pia na yeye alitumia nafasi hiyo kumnadi kwa kuwa barabara zilizojengwa Vunjo, zilitokana na kazi yake (Magufuli).
Alisema haikuwa jambo baya kwake kumnadi mgombea wa chama kingine kwa kuwa ni mtendaji mzuri na ana matumaini kwamba wananchi watanufaika. Akizungumzia matokeo ya uchaguzi na hujuma alizofanyiwa, Mrema alidai vilitumika vipeperushi vilivyokuwa vinaonesha vina alama ya ndiyo bila ya ruhusa ya msimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kwa mujibu wa Mrema, hakuwa mtu wa kushindwa katika uchaguzi huo kwa kuwa wananchi wake wanampenda na hawaamini matokeo ya uchaguzi huo. Wakati huo huo, aliyekuwa mgombea Urais wa TLP, MacMillian Lyimo alisema uvyama hautalifikisha taifa mahali pazuri isipokuwa kwa kuunda serikali ya Kitaifa.
Lyimo alisema, kitendo cha Mrema kumnadi Magufuli si tatizo bali ni ishara ya kuwa na serikali inayokubalika na vyama vyote. Mwenyekiti wa wanawake jimbo la Vunjo kupitia TLP, Venancia Msoya alisema Mrema aliwasaidia katika uongozi wake kwa kudhamini vikundi 43 vya wanawake na kuwa bega kwa bega na wananchi wa jimbo hilo. Alisema wanasikitika kuona kiongozi wao amekosa ubunge kwa hujuma alizofanyiwa na wapinzani wake.

Maoni