NDUGAI NA WENGINE SABA WAMINYANA USPIKA HII LEO


UCHAGUZI wa Spika wa Bunge la Tanzania unatarajiwa kufanyika leo ambapo wagombea wanane kutoka vyama tofauti wamejitosa kuwania nafasi hiyo katika Bunge la 11 linalotarajiwa kuanza leo mjini hapa.
Akizungumza mjini hapa jana, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema mwisho wa vyama vya siasa kuwasilisha majina kwenye ofisi yake ilikuwa jana saa 10 alasiri. 
 Aliwataja watakaopigiwa kura leo na vyama vyao katika mabano ni Peter Leonard Sarungi (AFP), Hassan Kisabya Almas (NRA), Dk Godfrey Rafael Malisa (CCK), Job Yustino Ndugai (CCM), Godluck Joseph ole Medeye (Chadema), Richard Shedrack Lyimo (TLP), Hashim Spunda Rungwe (Chaumma) na Robert Alexander Kasinini (DP).
 Kati ya wagombea hao, ni Ndugai peke yake ambaye ni Mbunge katika Bunge la 11 ambaye katika Bunge la 10 lililomalizika Agosti mwaka huu, alikuwa Naibu Spika. Ndugai ni Mbunge wa Kongwa tangu mwaka 2000. 
Kwa upande wa Ole Medeye amepata kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne na hadi Agosti alikuwa Mbunge wa Arumeru Magharibi kupitia CCM.

Alikihama chama hicho tawala Agosti mwaka huu, na alikuwa mshirika mkubwa wa mgombea urais kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Waziri Mkuu aliyejiuzulu mwaka 2008, Edward Lowassa. Kwa upande wake, Rungwe ambaye kitaaluma ni mwanasheria, aligombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kupitia Chaumma na mwaka 2010 aligombea kupitia chama cha NCCR-Mageuzi.
 Dk Kashililah alisema hadi kufikia mchana jana, wabunge 348 walikuwa wameshajisajili kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 11. Mapema jana, Ndugai aliibuka kidedea kuwania nafasi hiyo kwa CCM baada ya wagombea wengine wawili kujitoa.
 Juzi Kamati Kuu ya CCM iliteua majina matatu na kuyawasilisha kwenye Kamati ya Wabunge wa CCM ili yapigiwe kura kupata jina moja litakalopelekwa bungeni kupigiwa kura na wabunge wote kwa nafasi ya Spika leo.
 Pamoja na Ndugai, wengine walikuwa ni Abdullah Ali Mwinyi ambaye ni Mbunge wa Afrika Mashariki na Dk Tulia Ackson Mwansasu ambaye alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali mpaka jana alipoteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mbunge wa Bunge la Tanzania.

“Wagombea wengine wawili wamejitoa kwa sababu wana imani kubwa na Ndugai, hivyo kwa vile CCM ina wabunge wengi ambao ni sawa na asilimia 74.8 ya wabunge wote waliopo bungeni hadi sasa, hatuna shaka kwamba huyu atakuwa Spika,” 
alisema Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipozungumza na waandishi wa habari jana katika Ukumbi wa White House mjini hapa.
Akizungumza baada ya kupitishwa, Ndugai aliwashukuru wabunge wenzake na kwamba kama leo akichaguliwa atakuwa Spika atakayetenda haki kwa wabunge wote na atakuwa Spika bora. 
“Tumeambiwa kwamba ilikuwa ‘Hapa Kazi tu’, lakini kwa sababu tushaanza kazi tuseme ‘Sasa Kazi Tu’, nami itakuwa vivyo hivyo,” alisema Ndugai na kueleza kuwa Bunge la safari hii litakuwa na changamoto kubwa kwani lina wabunge wengi vijana na pia wasomi wameongezeka.
Awali, akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliwapongeza wabunge wa chama hicho kwa ushindi walioupata na kuwataka waendeleze kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ kwa kufupisha maneno ‘Sasa Kazi Tu’ kwa vile tayari wameanza majukumu yao. Uchaguzi huo ulisimamiwa na wajumbe wa Kamati Kuu ambao ni Jerry Silaa, William Lukuvi na Dk Maua Daftari.
Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama ambaye ni Mbunge wa Peramiho akizungumza kabla ya kumkaribisha Kinana, alisema wabunge wote wa CCM hadi sasa ni 252 na waliohudhuria jana walikuwa 228. 
Watanzania wengine waliowahi kushika nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania ni Adam Sapi Mkwawa kuanzia 1964 hadi Novemba 19, 1973, Chifu Erasto Mang'enya Novemba 20, 1973 hadi Novemba 5, 1975, Mkwawa tena kuanzia Novemba 6, 1975 hadi Aprili 25, 1994.
Wengine ni Pius Mseka Aprili 28, 1994 hadi Novemba 20, 2005, Samuel Sitta Desemba 26, 2005 hadi Novemba 2010, kisha Makinda Novemba 12 hadi leo atakapopatikana Spika mpya. 
Naibu Spika Uchaguzi wa Naibu Spika utafanyika Alhamisi wiki hii ambapo jana Muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulisema tayari ulikamilisha mchakato wa kupata mgombea wake.

Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene aliwaambia waandishi wa habari kuwa Ukawa watamsimamisha Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua mkoani Tabora. 
Alisema Ukawa walifanya vikao kadhaa kufikia uamuzi huo kuanzia ngazi ya vyama, wabunge na kisha viongozi wa juu na kupata majina mawili ambayo ni Ole Medeye kwa Uspika na Sakaya kwa Naibu Spika.
Kwa upande wa CCM, wenyewe walianza kutoa fomu jana, ambapo habari zilizopatikana jana ni kuwa wabunge saba wa chama hicho walikuwa wamejitokeza kuwania nafasi hiyo.
 Tofauti na ilivyokuwa katika mchakato wa Spika, ambapo wanaochukua fomu walikuwa wakitangazwa, hali ni tofauti kwa nafasi hiyo ambapo imeelezwa 
Kamati ya Wabunge wa CCM ndiyo inayosimamia.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, miongoni mwa waliojitokeza jana kuchukua fomu ni Dk Tulia na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu. 
Hata hivyo, Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo jana na kusema kuwa hawawezi kutaja majina wala idadi kwa sababu uchukuaji fomu bado unaendelea.

Alisema leo wabunge wa CCM watakutana kwa ajili ya kupiga kura kuchagua mbunge mmoja kati ya wabunge watakaojitokeza kwa ajili ya nafasi ya Naibu Spika.

Maoni