Katika hali isiyokuwa ya kawaida watu 5 kati ya 6 waliokuwa wamefunikwa na kifusi kwa siku 41 katika machimbo madogo wa Nyangalata wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameokolewa wakiwa hai.
Wakizungumza na Kahama Fm leo wakati wakiwa wamelazwa katika hospitali ya mji wa Kahama, wahanga hao wamesema hali hiyo imewakuta katika harakati za kuwaokoa wenzao waliokuwa wamefukiwa na kifusi katika machimbo hayo.
Wahanga hao ni Onyiwa Kanyimbo(55),Msafiri Jerald(38) Amosi Muhangwa(25), Chacha wambura(53) na Joseph Burule(44) na aliyefariki dunia ni Mussa Supana.
Wamesema walikuwa wakiishi kwa kunywa maji, vyura magome ya miti pamoja na mende hali iliyowasababisha kuendelea kuwa hai kwa siku 41 hadi jana jioni walipookolewa.
Meneja wa mgodi mdogo huo Amos Mbanga amesema timu ya mafundi ilifanya utafiti na kugundua kuna sauti za watu zikiita na kuamua kupeleka waokoaji kwa kushirikiana na serikali pamoja kampuni ya Acacia na kufanya uokoaji huo kuchukua masaa 24.
Naye kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Kahama Dk. Jibai Mkama amethibitisha kuwapokea wahanga hao na kwa sasa hali zao zinaendelea vizuri wakiwa bado wanapatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
Kwa upande wake katibu mkuu wa wachimbaji wadogo wa madini mkoa wa Shinyanga Bw. George Kibusy ametoa rai kwa yeyote atakayeguswa kutoa masaada wa hali na mali kwakuwa wahanga hao wana mahitaji makubwa ikiwemo nguo na chakula.
Ni jambo ambalo sio rahisi kuingia akilini na kueleweka binadamu kukaa chini ya ardhi kwa zaidi ya siku arobaini lakini watu hawa watano walijikuta wakiishi kwa kudura za mwenyezi mungu.
Maoni
Chapisha Maoni