KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ametoa ufafanuzi mpya kuhusu maagizo ya Rais John Magufuli, kwa watendaji wakuu na maofisa masuhuli wote wa wizara, idara na taasisi za Serikali, katika suala zima la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za umma.
Katika ufafanuzi huo uliotumwa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Balozi Sefue ametaka kila mtendaji wa Serikali kujihoji mwenyewe, kwamba endapo Rais Magufuli ataamua kufika katika eneo lake la kazi, ni kwa kiasi gani atakuta ametekeleza maagizo yake.\
“Rais ameonesha njia, sasa kwa wakati huu ni vyema kila Mtendaji Mkuu wa Serikali, ajiulize endapo Rais Magufuli atafika katika eneo lake la kazi, ni kwa kiasi gani atakuta nimetekeleza maagizo yake,” ameeleza Balozi Sefue katika ufafanuzi huo.
Akiingia kwa ndani, Balozi Sefue ametoa mfano wa uchapishaji wa kalenda na vitabu vya kumbukumbu (diaries) na kutaka kila Mtendaji Mkuu au Ofisa Masuhuli wa Serikali, apime mwenyewe kama ni lazima kutengeneza na kuchapisha vitu hivyo na kama kuna ulazima, wachapishe kwa kiasi gani.
“Ni matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kila wizara, idara na taasisi za Serikali kuchapisha idadi kubwa ya kalenda na diaries ambazo wakati mwingine hata hazitumiki mpaka mwaka unakwisha,” alisema Balozi Sefue.
Kadi, sherehe Ufafanuzi huo umekuja baada ya hatua mbalimbali kuchukuliwa na Dk Magufuli katika kubana matumizi ya fedha za Serikali yasiyokuwa ya lazima, ikiwemo kupiga marufuku utengenezaji na uchapishaji wa kadi za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya. Magufuli wiki hii alipiga marufuku wizara, idara au taasisi za umma kuchapisha kadi hizo kwa kutumia fedha za Serikali.
Badala yake, aliagiza fedha zilizopangwa kugharamia utengenezaji na uchapishaji wa kadi hizo, zitumike kupunguza madeni ambayo wizara, idara na taasisi hizo zinadaiwa na wananchi, wazabuni waliotoa huduma na bidhaa kwao au zipelekwe katika matumizi mengine ya kipaumbele. Mbali na kadi, pia alizuia kufanyika kwa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyotarajiwa kufanyika Desemba mosi mkoani Singida, na badala yake fedha za sherehe hizo zitumike kununulia dawa za kupambana na makali ya virusi vya Ukimwi kwa wagonjwa.
Safari za nje Ukiacha kuzuia uchapishaji wa kadi, Novemba saba mwaka huu, Rais Magufuli, alitangaza kuzuia safari za watumishi wa umma nje ya nchi, kutokana na ukweli kuwa safari hizo zimekuwa zikigharimu mabilioni ya fedha pasipo kuzingatia umuhimu kwa maslahi ya Taifa.
Kutokana na hatua hiyo, Rais aliamuru mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania, watumike kwenye mikutano ya kimataifa au shughuli zilizokuwa zikitakiwa kufanyika nje ya nchi.
Kwa waliokuwa na ulazima wa kwenda safari za nje, Rais Magufuli alitaka wafuate kibali kwake mwenyewe au kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue. Sherehe ya wabunge Jitihada za kuzuia matumizi ya Serikali za Dk Magufuli, zilifika mpaka kwa wabunge baada ya kuagiza fedha zilizochangwa kwa ajili ya kugharamia hafla ya kuwapongeza, zipelekwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kununulia vitanda vya wagonjwa.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kuwa, wadau mbalimbali walikuwa wamechanga Sh milioni 225 kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge katika siku ya uzinduzi wa Bunge. Alitoa maagizo kuwa kiasi kidogo tu cha fedha ndicho kitumike kwenye hafla hiyo na sehemu kubwa ipelekwe Muhimbili, ili zikatumike kununulia vitanda vya wagonjwa.
Siku chache baada ya uamuzi huo, fedha hizo zilitolewa na Katibu wa Bunge kwenda Bohari ya Dawa (MSD), ambao walinunua vitanda 300, viti maalumu vya wagonjwa 30, vitanda maalumu vya kubebea wagonjwa 30, mashuka 1,695 na mablanketi 400 kwa ajili ya wagonjwa. Sherehe za Uhuru Eneo lingine ambalo limekumbwa na hatua za kupunguza mapato ya Serikali, ni sherehe za miaka 54 ya Uhuru, ambazo zimekuwa zikifanyika Desemba 9, kila mwaka.
Rais Magufuli amezuia kufanyika kwa sherehe hizo mwaka huu na kuamuru siku hiyo itumike kufanya kazi ikiwemo usafi kwenye maeneo mbalimbali nchini, ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu. Kwa mujibu wa Rais Magufuli, wananchi hawapaswi kusherehekea miaka 54 ya Uhuru wa Tanzania Bara, huku wakiendelea kufa kwa ugonjwa huo unaosababishwa na uchafu.
Aidha, fedha zilizokuwa zitumike kugharamia sherehe hiyo, sasa zitapangiwa matumizi mengine ya maendeleo hususan kuboresha huduma za afya. Vikao kwa televisheni Hatua zingine za kupunguza matumizi zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na katazo la maofisa wa Serikali kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya vikao vya kazi, ambalo limewahusu wakurugenzi, makatibu tawala wa mikoa na wilaya pamoja na wafanyakazi wengine wa umma.
Badala yake watumishi hao wametakiwa kufanya mikutano kwa kutumia mfumo wa mawasiliano kwa njia ya video, ili kupunguza gharama za kuendesha vikao hivyo, kwa sababu washiriki wataunganishwa kwa mfumo wa video wakiwa kwenye vituo vyao vya kazi. Maofisa wa TRA Katika hatua nyingine, maofisa watatu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) ambao Waziri Mkuu Majaliwa Kassim, aliagiza juzi wahamishwe kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa mingine, jana aliwabadilishia maelekezo na kupewa adhabu ya kusimamishwa kazi.
Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, iliwataja maofisa hao kuwa ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.
“Kazi ya kuwachunguza ilianza jana ileile na sasa, tumeona hawa watu wanapaswa kuwa nje ya utumishi, ili kupisha uchunguzi ufanyike kwa uhuru zaidi,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa katika taarifa hiyo. Pia Waziri Mkuu amemuagiza Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango atekeleze maagizo hayo kwa kuwaandikia barua watumishi hao.
Kwa hatua hiyo, watumishi waliosimamishwa kazi mpaka jana, wamefikia tisa kutokana na kashfa ya kupotea kwa makontena 349 yaliyopita bandarini, lakini hayakulipa kodi ya Serikali yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 80.
Wengine waliosimamishwa kazi juzi ni pamoja na Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade, aliyechukuliwa hatua hiyo na Rais Magufuli na nafasi yake kukaimiwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Mpango.
Waliowekwa mahabusu Mbali na hao wanne ambao wamesimamishwa kazi tu na kuzuiwa kusafiri nje ya nchi, kwa kunyang’anywa hati zao za kusafiria, Waziri Mkuu Majaliwa pia juzi aliwasimamisha vigogo wengine kazi, lakini adhabu yao ikawa kubwa kidogo baada ya kukabidhiwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu.
Vigogo hao waliosimamishwa na kuwekwa rumande ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki, Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya, Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari (hakutaja ni wa idara gani) na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In-Charge), Eliachi Mrema
Maoni
Chapisha Maoni