RAIS mteule, Dk John Magufuli anatarajiwa kuapishwa rasmi leo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sherehe zitakazofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru uliopo jijini Dar es Salaam.
Kwa mara nyingine, Tanzania itakuwa inabadilisha uongozi wake wa juu kwa amani na utulivu tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aondoke madarakani kwa hiari yake mwaka 1985 baada ya kuiongoza nchi kwa miaka 23. Baada ya kung’atuka kwake, Katiba ilibadilishwa na kutoa fursa ya kuongoza kwa mihula miwili ya miaka mitano mitano kwa maana rais aliyepo anaweza kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili.
Dk Magufuli (56) anachukua nafasi hiyo ya urais kutoka kwa Rais anayemaliza muda wake, Jakaya Kikwete ambaye anaondoka madarakani kikatiba baada ya kumaliza mihula miwili ya miaka 10. Dk Magufuli ambaye alikuwa Waziri wa Ujenzi katika Serikali ya Rais Kikwete, anaapishwa leo kuwa Rais wa Awamu ya Tano baada ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Katika uchaguzi huo, akipeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alichuana na wagombea wengine saba, huku mshindani wake wa karibu akiwa ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye alikuwa mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Dk Magufuli alishinda kwa kupata kura 8,882,935 ambayo ni sawa na asilimia 58.46 huku mpinzani wake aliyemfuata kwa karibu, Lowassa akipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 kutoka kwa wapigakura milioni 15.5 kati ya wapigakura milioni 23.7 waliojiandikisha kupigakura.
Akishakuapa mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman, Dk Magufuli atakuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa ni rais wa kwanza mwanasayansi na msomi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) kukalia Ikulu ya Magogoni. Daktari huyo ambaye ameoa na ana watoto, alifundisha masomo ya Kemia na Hisabati katika Shule ya Sekondari ya Sengerema mkoani Mwanza katika miaka ya 1980 na kisha kufanya kazi katika Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza jijini Mwanza akiwa mkemia.
Ametanguliwa katika Ikulu na marais Kikwete, Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, na kwa mujibu wa Katiba, anaruhusiwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili mwaka 2020 atakapomaliza muhula wake wa kwanza anaouanza leo. Leo ni sikukuu Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alisema kutokana na sherehe hizo za kuapishwa kwa Dk Magufuli, Rais Kikwete ametangaza kuwa leo ni sikukuu na siku ya mapumziko.
“Rais amefanya uamuzi huo ili kuwawezesha Watanzania kushiriki katika sherehe za kuhitimisha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne na kuingizwa madarakani Mheshimiwa Dk Magufuli, kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Sefue. Sefue alisema Rais Kikwete ameitangaza leo kuwa siku ya sikukuu na mapumziko kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha Tatu cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa.
Milango wazi saa 12 asubuhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kuhudhuria sherehe hizo leo, ambapo milango ya Uwanja wa Uhuru, itakuwa wazi kuanzia saa 12 asubuhi. Alisema kwa mujibu wa ratiba ya awali, wageni waalikwa wanatarajiwa kuhudhuria sherehe hizo, kuanzia saa mbili asubuhi ambapo saa tatu asubuhi, marais waalikwa na wageni wa kimataifa wataanza kuingia wakiwemo viongozi mbalimbali nchini pamoja na Rais Kikwete na Dk Magufuli.
Alisema sherehe hizo zitanogeshwa na burudani nyingi, ikiwemo Rais Kikwete kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride kwa ajili ya kumuaga rasmi na pia Dk Magufuli naye atapigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride ikiwa ni ishara ya kumkaribisha madarakani Amiri Jeshi Mkuu huyo mpya. Aidha, Sadiki alisema pia sherehe hizo zitapambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo wa kizazi kipya, ngoma za asili, ndege za kivita, gwaride la heshima pamoja na kwaya.
Alisema mpaka sasa takribani nchi 42 pamoja marais wanane kutoka nchi mbalimbali, mabalozi na wanasiasa ndani na nje wamethibitisha kuhudhuria sherehe hizo. Wageni watakaohudhuria Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa, iliwataja marais watakaohudhuria sherehe hizo za uapisho kuwa ni Robert Mugabe wa Zimbabwe, Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda) na Jacob Zuma (Afrika Kusini).
Wengine ni Rais Joseph Kabila (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), Uhuru Kenyatta (Kenya), Filipe Nyusi (Msumbiji) na Edgar Lungu (Zambia). Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa zipo nchi zitakazowakilishwa na wakuu wake wengine wa nchi ambapo Malawi itawakilishwa na Makamu wa Rais, Saulos Chilima na Namibia Naibu Waziri Mkuu, Netumbo Nandi-Ndaitwah.
Aidha, baadhi ya nchi zilizothibitisha kuhudhuria sherehe hizo leo ni Norway, Oman, Sudan Kusini, Sweden, Umoja wa Falme za Kiarabu, Marekani, Uingereza, Shelisheli, Swaziland, Algeria, Misri, Benin, Denmark, Ethiopia, Finland, Ufaransa, Ghana, India, Japan, Kuwait, Uholanzi na Nigeria. Taarifa ya Polisi Kwa upande wa Jeshi la Polisi, kupitia Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Makao Makuu ya Polisi, Paul Chagonja, jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine, litahakikisha kunakuwa na usalama wa raia na mali zao.
“Jeshi la Polisi linawataka wananchi nchini kote kuendelea kuheshimu sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vya aina yoyote ile ambavyo vinaweza kuhatarisha usalama wa raia na mali,” alisema. Alisisitiza kuwa jeshi hilo, halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu au kikundi chochote, kitachoonesha viashiria vya uvunjifu wa sheria au kutaka kuvuruga amani ya nchi.
Maoni
Chapisha Maoni