Ushindi wa Chama cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 unabaki na utaendelea kubaki kuwa funzo kubwa tofauti na chaguzi zilizopita. Tanzania ilirejesha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi mwaka 1992 baada ya kuufuta miaka ya sitini mwanzoni. Mfumo wa vyama vingi ulirejeshwa baada ya serikali kuwahoji wananchi kupitia Tume ya Jaji Nyalali ambaye pamoja na mambo mengine alihoji wananchi kama Tanzania ilikuwa tayari kuingia katika siasa za vyama vingi.
Katika hali ambayo ilishangaza wengi miongoni mwa wasomi na wananchi wa daraja la kati na juu, wananchi kwa zaidi ya asilimia 80 walipendekeza mfumo wa chama kimoja uendelee. Kipindi kile busara na hasa ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwemo Mwalimu Nyerere walionelea ni vema tukaingia katika mfumo wa vyama vingi. Msingi wa busara na hekima hii ilitokana na ukweli kwamba katika maoni ya wale wananchi wengi waliopendekeza mfumo wa vyama vingi uendelee walitoa mapendekezo makubwa ambayo iwapo yangefanyiwa kazi ipasavyo tusingeweza kuwa tena na mfumo wa chama kimoja.
Wengi ya wana CCM kipindi kile hawakuonesha kufurahishwa na hatua ile kwasababu tayari kulikuwa na hali ya mazoea, kwa maneno mengine chama ndio kilikuwa kila kitu. Chama kilikuwa katika kipindi chote hadi mwaka 1992 kimeshika hatamu au “party supremacy”, kimsingi Serikali ilipata maelekezo kutoka katika chama na halkadharika Bunge nalo lilipata msukumo mkubwa kutoka katika chama. Mfano mzuri wa Chama kushika hatamu ulijidhihirisha wakati wa vuguvugu la G55 yaliyopelekea Bunge kupitisha azimio la kuundwa kwa serikali ya Tanganyika.
Baafa ya mjadala mzito wa ndani ilikubalika kwamba sera ya Chama cha Mapinduzi ni Serikali Mbili na ni uamuzi uliopitishwa na chama tena kwa turufu ya wanachama wenyewe. Ukiachilia mbali kwamba uamuzi ule wa Bunge ulighubikwa na mihemko ambayo haikuwa imetaarifiwa sawasawa na uhalisia. Baada ya vuta-nikuvute uamuzi wa chama ulitamalaki na maisha yakaendelea.
Mwaka 1995 ndio ilikuwa Uchaguzi Mkuu wa kwanza katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Uchaguzi wa mwaka 1995 ulikuwa na changamoto na mhemko mkubwa kama huu wa miaka 20 baadaye yaani mwaka 2015. Ikumbukwe mwaka 1995 Naibu Waziri Mkuu aliondoka CCM akahamia chama cha upinzani kipindi hicho. Kampeni zilichagizwa na mihemko na mashamsham kama ya mwaka huu. Kipindi hiki naona watu wanajitambua zaidi kwamba baada ya mkutano gari ya Mhe. Lowassa iliachwa itembee yenyewe kuelekea nyumbani kwake baada ya mkutano. Mwaka 1995 gari ya Mhe. Agostino Lyatonga Mrema haikuachwa iwashwe na kutembea yenyewe, bali ilisukumwa mpaka nyumbani kwake.
Ikumbukwe pia mwaka 1995 mgombea wa CCM, Mzee Mkapa hakuwa almaarufu katika CCM, na yeye ni kama alifichuliwa kutoka kwenye kona iliyofichika ya jukwaa kubwa na pana la CCM. Kipindi kile walikuwapo magwiji katika chama cha mapinduzi ambao kwa rafu nyingi walitamani wapewe dhamana ya kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa kwanza katika demokrasia ya vyama vingi. Kwa sauti moja CCM ilikataa hadaa na kwa kiasi msukumo wa Mwalimu Nyerere.
Mwalimu Nyerere alizunguka huku na huko akimuuza Mhe. Mkapa kwa watanzania, na nikiri kwamba heshima waliyokuwa nayo kwake ilikuwa mtaji wa kura zilizompa Mhe. Benjamin Mkapa dhamana ya kuwa Rais wa Jamhuri yetu. Kwa upande mwingine CCM ambayo tayari Mwalimu alikuwa ameshaikosoa sana kipindi kirefu cha miaka ya 90 mwanzoni kwa kupungukiwa uadilifu, lakini kwa tiketi ya ndugu Benjamin Mkapa aliyekuwa tunu ing’aayo na iliyouzwa na Mwalimu mwenyewe chama kikaponea hapo na kuvuka na ushindi.
Mheshimiwa Mkapa alifanya vizuri sana awamu yake ya kwanza ambayo iliwezesha ushindi wake katika awamu ya pili kwa maana ya uchaguzi wa mwaka 2000.
Mwaka 2005, kilichoipa CCM ushindi ilikuwa kampeni nzuri ya kisayansi na iliyochagizwa na tiketi ya ujana kama sehemu ya mabadiliko ya kirika ndani ya Chama cha Mapinduzi lakini pia hilo likiwa ni sehemu ya kiu ya watanzania kipindi kile. Wengi mtakubaliana name kwamba “ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya” yalikuwa maneno yaliyoongeza hamasa ya ushiriki wa vijana katika kuleta mabadiliko katika CCM. Leo sio kusudio langu kujadili namna mchakato wa kumpata mgombea wa CCM mwaka 2005 lakini kusudio langu ni kuonesha katika kila uchaguzi namna ambavyo CCM imeweza kupenya ukiachilia upinzani mkali kutoka vyama vyenye mawazo mbadala nchini.
Ipo ile desturi ya Chama cha Mapinduzi kwamba akipewa mtu nafasi ya Madaraka ya Urais kwa awamu ya kwanza (miaka mitano) basi apewe pia na awamu ya pili ili akamilishe kazi aliyopewa na kutimiza miaka 10. Kwa sehemu imeonekana kuwa desturi ambayo mpaka mwaka 2010 wananchi wa kawaida walionesha kukubaliana nayo. Hili linaonekana kupotea kipindi hiki na kadri muda unavyoendelea hasa ukizingatia wapiga kura wengi kipindi hiki na mwaka 2020 watakuwa ni vijana chini ya miaka 40 ambao wengi wao wamepata elimu ya msingi mpaka kidato cha nne.
Nikiongea na wengi ya vijana hawa utawasikia wakisema “tunampa miaka mitano akiboroga toa tupa kule na tunaweka mwingine”. Huenda ile busara ya kumwachia mtu amalize na kipindi cha pili inaweza isiendelee katika chaguzi zinazofuata. Hili ni funzo kubwa la kwanza kwa CCM kwamba ile dhana kwamba wananchi watatoa dhamana kwa awamu ya pili ili kutimiza miaka 10, kwa kipindi hiki na chaguzi zinazofuata kama hatutafanya kazi ambazo zitaonekana miongoni mwa watanzania basi tujiandae kisaikolojia kushindwa.
Uchaguzi wa Mwaka 2015, kama ule wa Mwaka 1995 zinashabihiana kwa ukaribu sana. Tofauti na mwaka ule ilikuwa Naibu Waziri Mkuu Mhe. Mrema aliyehamia upinzani, mwaka 2015 ni Mawaziri Wakuu wawili, Mhe. Lowassa na Mhe. Sumaye. Mgombea wa CCM ni kama alivyokuwa Mkapa mwaka 1995, ameonekana si mjuvi wa siasa za ndani za chama hadi kufikia baadhi ya makada wa CCM kumtamka hadharani kwamba hajui siasa. Ukiacha beza beza za baadhi ya wana CCM kama ilivyokuwa kwa Mkapa, kipindi hiki aliyekuwa nuru inayong’aa na inayouzika kwa wapiga kura wa kipindi hiki si mwingine bali ni Dkt. Magufuli.
Kipindi hiki Mwalimu hayuko lakini viongozi wote wakubwa wastaafu na hasa wale ambao watanzania wanawaona wana akisi haiba ya Mwalimu Nyerere, nawazungumzia Mzee Joseph Sinde Warioba, Dkt. Salim Ahmed Salim na hata Mama Maria Nyerere wameonesha kumuunga mkono Dkt. Magufuli moja kwa moja.
Mchezo ambao CCM ilifanya ikiwemo kuwaruhusu baadhi ya makada wake waliokuwa wanautafuta urais wa kimungu chini ya Katiba ya mwaka 1977 wakavuruga mchakato wa Katiba Mpya ambao wananchi wenyewe walitoa maoni yao. Kura za CCM kipindi hiki zimepunguzwa kama sehemu ya adhabu ya kupuuza maoni ya wananchi katika mchakato wa Katiba. Nakiri kusema asingekuwa Dkt. Magufuli, CCM ilikuwa haiuziki tena. Nakiri kusema hii ndio tiketi ya mwisho. Iwapo CCM haitaamka na kuwajibika mchana na usiku hakika 2020 itatukuta nje ya Bunge na nje ya Ikulu.
Maoni
Chapisha Maoni