WIKI YA KIHISTORIA NCHINI TANZANIA





HISTORIA mpya inaandikwa wiki hii mkoani Dodoma ambako Bunge la 11 la Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais John Magufuli linatarajiwa kuanza vikao vyake kesho.
Wiki hii Watanzania watashuhudia upatikanaji wa Spika mpya pamoja na Naibu wake, na pia ni mwanzo wa mikutano ya Bunge jipya, lakini pia ni wiki ambayo Bunge litathibitisha jina la Waziri Mkuu wa 11 wa Tanzania ambaye kwa vyovyote atakuwa ni mpya.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, kuanzia Ijumaa hadi jana ilikuwa usajili kwa wabunge wote wanaotarajiwa kushiriki Bunge hilo na leo kuanzia saa nne asubuhi hadi saa sita mchana, itakuwa kikao kwa wabunge wote na kisha watatembelea Ukumbi wa Bunge.
Ratiba inaonesha kuwa alasiri kutakuwa na mikutano ya kamati za vyama na hiyo itakuwa mahususi kwa ajili ya kuchagua mgombea Uspika kupitia chama husika. Kesho Jumanne itakuwa ni kuanza kikao cha kwanza cha Bunge na kusomwa Tangazo la Rais la kuitisha Bunge ambapo pia kutafanyika uchaguzi wa Spika na kisha ataapishwa.
Baada ya tukio hilo, utapigwa Wimbo wa Taifa na baadaye wabunge wataanza kuapishwa shughuli itakayoenda hadi Alhamisi asubuhi. Alhamisi jioni itakuwa kuthibitisha jina la Waziri Mkuu ambapo Spika atakuwa amepokea jina hilo kutoka kwa Dk Magufuli na baadaye kutafanyika uchaguzi wa Naibu Spika.
Ratiba inaonesha Ijumaa alasiri Rais Magufuli atahutubia Bunge na baadaye itatolewa hoja ya kuahirisha Mkutano huo wa Kwanza wa Bunge la 11. Uchaguzi wa Spika Joto la uchaguzi wa spika limekuwa likipanda kwa kiasi fulani ambapo tangu Ijumaa wabunge walivyoanza kujisajili, kila aliyehojiwa na vyombo vya habari amekuwa akitaja sifa za mtu anayeona akiwa nazo anastahili kuwa spika mpya.
Sifa kubwa zimekuwa ni uzoefu, kujua kanuni, masuala ya kisheria, lakini wengi wameenda mbali wakitaka spika mpya awe yule mwenye utayari wa kuyakabili mabadiliko, lakini pia asibanwe na itikadi za vyama.
Jana na leo vyama vinavyotarajia kusimamisha wagombea uspika vilikuwa vikiendelea na mchakato wa namna ya kuwapata wagombea hao ambapo ni Samuel Sitta pekee ambaye amewahi kushika wadhifa huo katika Bunge la Tisa, anawania kuteuliwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hata hivyo, Sitta amekwama katika uteuzi huo, na sasa nafasi hiyo itakuwa na wagombea wapya pekee, hivyo nchi kuingia katika historia ya kuwa na Spika mpya kwani wa sasa, Anne Makinda ametangaza kustaafu siasa.
Watanzania wengine waliowahi kushika nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania ni Adam Sapi Mkwawa kuanzia 1964 hadi Novemba 19, 1973, kisha aliingia Chifu Erasto Mang’enya Novemba 20, 1973 hadi Novemba 5, 1975, kisha akarudi tena Mkwawa kuanzia Novemba 6, 1975 hadi Aprili 25, 1994.
Wengine ni Pius Msekwa kuanzia Aprili 28, 1994 hadi Novemba 20, 2005, Sitta kuanzia Desemba 26, 2005 hadi Novemba 2010, kisha Makinda kuanzia Novemba 12 hadi kesho atakapopatikana spika mpya.
Upatikanaji wa Waziri Wakuu Tukio lingine wiki hii ni la Waziri Mkuu ambaye atakuwa mpya kwa vile kwa mujibu wa Katiba, lazima Waziri Mkuu awe miongoni mwa wabunge wanaotokana na majimbo na katika wabunge waliopita hakuna ambaye alishawahi kuwa Waziri Mkuu.
Rais Magufuli atawasilisha kwa Spika jina la Waziri Mkuu ambalo litathibitishwa kwa kupigiwa kura na wabunge. Mawaziri wakuu 10 waliopita ni Mwalimu Julius Nyerere, Rashidi Kawawa, Edward Sokoine (wote marehemu), Cleopa Msuya, Dk Salim Ahmed Salim, Joseph Warioba, John Malecela, Frederick Sumaye, Edward Lowassa na Mizengo Pinda.
Kitendawili cha nani atakuwa Waziri Mkuu wa 11 wa Tanzania katika Bunge la 11 kitateguliwa wiki hii, ambapo katika viwanja vya Bunge kwa siku tatu ambazo usajili unafanyika, baadhi ya wabunge wamekuwa wakitaka kuitana majina hutaniana kwa kuanza na neno Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Maoni