Mohamed hamad akifanya mahojiano na mzee Kibati wa kibaya juu ya changamoto za walemavu Mkoani Manyara.
Walemavu na changamoto za kulijenga Taifa
MOHAMED HAMAD.
WALEMAVU ni kundi maalumu
lililopo ndani ya jamii, kundi hili limesahaulika hali inayotishia ustawi wa
maisha yao kutokana na kukosa mahitaji
mbalimbali ya kuwezesha waishi ama kuchangia maendeleo yao na Taifa
Kila mtu ana haki na wajibu
katika nchi yake kuchangia maendeleo bila kujali jinsia yake kwa hali na mali, lakini katika kada hii inahitaji msaada
mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo serikali ili kuwezesha kufanikisha malengo
yao
Walemavu wamegawanyika katika
makundi mbalimbali, yakiwemo wasioona, wenye upungufu wa viungo, walemavu wa
ngozi, walemavu wa mtindio wa ubongo, na viziwi ambao kila kundi linatamani
kuchangia maendeleo ya Taifa lao
Katika michango hiyo wengi
wao wanashindwa kuchangia kutokana na aina ya ulemavu walio nao, hivyo kuomba
msaada kwa wadau na hasa Serikali ili waweze kufikia ndoto zao ambazo zinazidi
kufifia siku hadi siku
Makala hii inajikita kuona
ushiriki wa walemavu katika uchaguzi na changamoto zinazowakabili kwa zoezi hilo ambalo ni muhimu
katika mustakabali wa nchi katika kuchagua na kuchaguliwa
Akizungumzia nafasi ya
walemavu kuchangia maendeleo Bw. Ramadhani Athumani Konki mlemavu wa kutosikia
wilayani Kiteto alisema, walemavu wanashindwa kushiriki kuchangia shughuli za
maendeleo kwa kutokuwa na elimu ya ushiriki kwenye maendeleo hayo
“Walemavu wanahitaji kupatiwa
elimu ya utambuzi na mawasiliano ya lugha za alama ili waweze kushiki na jamii
vyema katika masuala ya kijamii ambayo yanawezesha Taifa kusonga mbele”alisema
Konki
Alisema mbali na changamoto hizo
pia wamekuwa wakibaguliwa kwa misingi ya hali walizonazo kwa kuonekana kuwa
hawawezi kuchangia maendeleo ndani ya jamii na Taifa kwa ujumla jambo ambalo
wanaona kuwa hawatendewi haki
Alisema walemavu wanashindwa
kushiriki kikamilifu katika vyombo vya maamuzi kama vikao na makongamano
yanayoshushirikisha umma katika maendeleo yao
kutokana na mtazamo hasi wa jamii pamoja na mifumo duni ya mawasiliano yaliyopo
kati yao na
wadau hao
“Huwezi kuomba nyadhifa
mbalimbali za uongozi ndani ya jamii, kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo
ubaguzi na unyanyapaa, kutokana na aina ya ulemavu tulionao sisi
walemavu”alisema
Alisema kumekuwepo na ushiriki
hafifu wa walemavu katika hatua mbalimbali za uchaguzi zikiwemo mikutano ya
kampeni hali inayofanya wakose haki zikiwemo kuchagua na kuchaguliwa
“Mlemavu wa macho anahitaji
kushikwa mkono kwenda kwenye mkutano, halikadhalika viziwi anahitaji kutafsiriwa
kinachozungumzwa, kukosekana kwa vifaa vya mawasiliano kumechangia tuwe nyuma
kwa kila jambo”alisema Konki
Pia huduma hiyo ikikosekana mlemavu
hawezi kuendana na mtu mwengine asiye na ulemavu anayeomba nafasi ya uongozi
kwa kufanya ushindani kwa namna yoyote ile ni lazima mlemavu atakosa nafasi kutokana
na hali yake, alisisitiza Konki
“Awali tuliona tafsiri ya
lugha za alama kwenye baadhi ya vyombo vya habari kama
vile TV ingawa wengi wetu hatukuwa na uelewa wa mawasiliano hayo kwa kutokuwa
na elimu ya ufahamu wa lugha hiyo lakini ilisaidia, sasa hivi hakuna tafsiri
inayotolewa kwa walemavu kwenye vyombo hivyo”
Naiomba Serikali kusaidia kukata
mirija ya ubaguzi na kuwezesha upatikanaji wa elimu ya lugha ya alama kwa
walemavu ili kuongeza wigo wa walemavu kushiriki maendeleo kwa ujumla, alisema
Konki huku akionyesha kukasirishwa kwa kukosa huduma hiyo
Kassimu Ismail Kibati mlemavu
wa masikio na kuona alisema, tatizo la Serikali ni kukosekana kwa mfumo imara
wa kuwawezesha walemavu kushiriki katika maendeleo ya jamii japo kutoa mapendekezo
ya namna ya kusaidiwa “Huwezi kuwazungumzia walemavu wakati huwaoni”alisema
“Ukiangalia hata miundombinu
ya majengo ya umma sio rafiki kwa walemavu mfanoss walemavu wa viungo, hali
tunayohisi kuwa huo ni ubaguzi wa wazi na ambao unatenga kundi hili ili
wasiweze kunufaika na fursa mbalimbali”alisema Kibati
“Kuna mifano hai ya maeneo
yetu , tuna viongozi wanaosimamia wasichokiamini kuna miradi mingi ya ujenzi wa majengo ya umma
hakuna miundombinu rafiki kwa walemavu kuingia wakiwa huru kwenda kwa watawala
wao na badala yake wanalazimika kupata usaidizi kuwafikia watawala”
Mmoja wa waalimu wa shule ya msingi
Kibaya ambaye hakutaka kutaja majina yake gazetini alisema, kuna idadi kubwa ya
watoto wenye mahitaji maalumu ambao hawajaandikishwa shule kutokana na Serikali
kutokuwa na dhamira ya dhati kusaidia kundi hilo kwa kuanzisha shule maalumu
“Huwezi amini hapa shuleni tuna wanafunzi 10 tu ambao ni viziwi lakini
kuna walemavu ambao hawajaanzishiwa kitengo kama
vile wasio ona na wenye mtindio wa ubongo ambao wazazi wamekata tamaa kuwa
watoto hao hawawezi kusoma tena””alisema mwalimu huyo
Alisema pamoja na kugundua
hili niliweza kuzungumza na wadau mbalimbali wa elimu lakini walishindwa kuchukua
hatua kutokana na suala hilo
kuwa linahitaji ufadhili mkubwa wa kupata waalimu,vyumba vya madarasa na vifaa
vya kujifunzia na kufundishia
Mwisho
Maoni
Chapisha Maoni