Changamaoto za wafanya biashara katika barabara

Na, MOHAMED HAMAD

SEKTA  ya biashara hapa nchini, imekuwa msaada mkubwa kwa  wananchi, ingawa wengi wao hawana uelwewa wa kutosha juu ya sekta hiyo,.. watu wengi wameneemeka na biashara kwa kuendesha familia zao.

Katika sekta hiyo, wapo wanaosomesha watoto kwa kufanya shughuli hiyo, ili hali maisha yasonge mbele kama ilivyoelekezwa na Serikali kuwa kila mtu anapaswa kufanye kazi ili mradi iwe ya kumpa kipato halali.

Wakati wananchi wakifanya biashara hiyo, Serikali nayo hupata  kipato kwa kutoza kodi, ambayo huwa ndiyo inayowezesha miradi ya maendeleo ya wananchi ikiwemo maji, afya, elimu pamoja na miundombinu ya barabara.

Hivi karibuni katika kikao cha baraza la biashara kilichofanyika wilayani Kiteto mkoani Manyara,  miongoni mwa changamoto zilizotajwa kuwakabili wafanya biashara hao ni pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wafanya biashara hao walimweleza Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magessa, kuwa pamoja na kuichangia Serikali kwa kulipa kodi hawanufaiki na fedha zao hizo kutokana na serikali kutotengeneza miundombinu ya barabara kwa kiwango cha kuridhisha.

Wamesema katika biashara zao, walitumia magari ya tani 30 kusafirishia mizigo, lakini  sasa wanalazimishwa kutumia magari ya tani 10, kulingana na barabara zilizopo hali inayowagharimu fedha nyingi kukodisha magari yanayoendana na barabara hizo ya tani 10

Mwenyekiti wa baraza la biashara wilayani Kiteto, Kanti Greogory, mbele ya mkuu wa Wilaya ya Kiteto Tumaini Magessa, alisema kuna kila sababu ya Serikali ya Kiteto kuomba barabara hizo kupandishwa hadhi .
Alisema barabara ya Kiteto- Arusha, Kiteto-Kondoa, Kiteto- Handeni, pamoja na ile ya kwenda Dodona, zimeharibika vibaya, na kwamba mvua za mwanzo mwaka huu zikianza uwezekano wa magari makubwa  kuingia Kiteto utakuwa ndoto.

Alisema ili wafanyabiashara waone kuwa hela yao wanayokatwa kodi inafanya kazi, Serikali haina budi kuhakikisha kuwa wanaboresha miundombinu ya barabara, sambamba na huduma zingine zinazohitajika ndani ya jamii.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magessa, aliwaambia wafanyabiashara hao kuwasilisha maombi hayo kwenye kikao cha baraza la biashara la mkoa, ili yaweze kuwa na nguvu ya kisheria.

“Ninachofahamu ni kwamba barabara za Kiteto zote zinauwezo wa kubeba tani 10, lakini magari ya tani 30 ndio yamekuwa ya kuitumia na kusababisha uharibifu, ambapo alimtaka mkurugenzi kuwa na sheria ndogo kudhibiti magari hao”.

Hata hivyo alisema, aliletewa sheria ambayo alipaswa kuipitisha kuwa aidha aruhusu magari ya tani 30 kupita wilayani humo na kuruhusu yale ya tani 10, jambo ambalo alisema amelazimika kutoisaini kwanza mpaka akutane na wadau kujua changamoto zinazowakabili.

Naye katibu tawala wa wilaya ya Kiteto, Ndaki stephano, akizungumza kwenye baraza hilo la biashara alishauri mkurugenzi mtendaji, Tamimu Kambona kuwa ili kunusuru barabara hizo, hana budi kuwa na barabara za kupitisha magari hayo makubwa nje ya mji

Alisema maeneo mengine, waliweza kunusuru barabara zao kwa kuwa na barabara maalumu za kupitisha malori makubwa na kuacha barabara za kati zikitumik kulingana na magari yaliyoruhusiwa ambayo ni tani 10

Naye Elieta Nanyaro (mfanyabiashara) aliutaka uongozi wa Wilaya ya kiteto kuwa wapana katika miundombinu, kuacha kufikiri barabara za ndani peke yake kwani barabara zitakapoimarishwa uwezekano wa wafanyabiashara kufika kiteto ni mkubwa

“Hatuwezi wanakiteto tukajifungia kwa kuangalia barabaza za ndani pekee, tunaweza kushirikiana na weneztu wa wilaya za jirani kuwa na barabara za kufikika kwa lengo la kutandaa kila kona ya nchi, na wakati huo Serikali nayo itapata mapato”

Awali Joseph Mwaleba, Afisa maendeleo ya Wilaya ya Kiteto, akichangia mada hiyo alisema, Wilaya haina sababu ya kuzungumzia barabara za nje kwakuwa hawana uwezo nazo, akisisitiza kuwa kuna barabara za Halamshauri na zile za Tanroad (serikali)

 “Ndugu zangu wafanya biashara tusiwe na wazo la kuzungumzia barabara za wenetu huko, tuanze na zetu za ndani ili tukiboresha watu watazitumia ipasavyo, tusitapetape na barabara za nje”

 Akifafanua hilo katibu wa baraza la biashara, Gusto Emmily aliwaasa viongozi wa Serikali kuwa na maono ya mbali akisema, kiongozi makini ni yule mwenye mtazamo ya siku za baadaye, akiwataka kutofikiria Kiteto bali wafikiri Tanzania zaidi

 Kuhusu eneo la viwanda ambalo wafanya biashara hao wanataka kutengewa na halmasahuri alisema kiasi kilichotengwa na wilaya ekari saba hazitoshi, na kumtaka mkurugenzi mtendaji kuona umuhimu wa sekta hiyo katika jamii

 “Ekari saba..hata mfanyabiashara mmoja wa mashine ya aliizeti hazimtoshi..wilaya angalieni na kufikiri upya juu ya maeneo ya uwekezaji, kutenga ekari saba ni sawa na kuonyesha sekta hii haina tija kwenu”alisema katibu huyo wa baraza la biashara Kiteto

 Katika hatua nyingine wafanyabiashara hao walishangazwa na maamuzi yaliyofanywa na baraza la madiwani, kuacha ujenzi wa soko la wilaya lililoungua na kutaka kuanzisha soko jipya jambo ambalo linawapa hofu kuwa huenda kuna janjajanja za kutaka kuhujumu fedha ya Serikali

Mwisho

Maoni