RC Manyara, vaa viatu vyako sasa

                                      Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dr, Joel Nkaya Bendera

Tanzania ni nchi inayoongozwa kwa misingi ya sheria kanuni na taratibu, kila mtu anapaswa kuheshimu sheria ili kuleta usawa katika nyanja ya upatikanaji wa amani, sambamba na kuitambua mihimili mikuu mitatu ya Dola, Serikali, Bunge na Mahakama

Kwa kawaida utulivu wa nchi husika, unategemea nidhamu ya wananchi katika kuheshimu sheria na taratibu za nchi hiyo, kwa maana nyingine ni kuwapa viongozi wao nafasi ya kutawala ili kuwaletea maendeleo badala ya kila siku kutatua migogoro ambayo wakati mwingine madhara hujitokeza

Ninayasema haya nikiamini hapatakuwa na maendeleo katika Taifa lolote kama hakuna amani, badala yake kila siku watu watakuwa katika harakati za kunusuru maisha na mali zao kukimbia huku na kule

Haya nimeyaona miaka minne iliyopita Wilayani Kiteto, ilijitokeza migogoro ya wakulima na wafugaji, nilishuhudia watu wakipoteza maisha na wengine mali huku wakiishi kwa wasiwasi mkubwa kuhofia maisha yao

Hali hii hata mimi nilitishika sana, tukawa tunaishi kwa hofu kubwa, na hasa kwa hali ya uelewa wangu niliona kilichosababisha ni kutotii sheria, na Serikali kutochukua hatua za haraka yanapojitokeza matatizo kwa wananchi

Kwa mara ya kwanza katika migogoro hiyo, niliwahi kuona katika chombo kimoja cha habari , watu wakitoa matamko wakiwa kama viongozi wa mila kuwa hawako tayari kuona jamii moja (wakulima) wakifanya kazi katika maeneo flani eti ni hifadhi

Kwa mujibu wa sheria na miongozo mbalimbali ya Serikali kuhusu hifadhi, hairuhusiwi mtu yoyote kufanya shughuli za kibinadamu katika hifadhi hizo, tofauti na utaratibu wa Kiteto kuwa jamii ya kifugaji (wamasai) wamekuwa wakitetea maeneo hayo na kuyatumia kama ilivyo, Hifadhi ya Emboley Murtangos, Hifadhi ya jamii ya WMA, SULEDO na sasa KIMOTONGE

Nikawa na maswali mengi yajiuliza wakati huo, kwanini jamii moja iwe inakataza jamii zingine kufanya shughuli za kilimo badala ya Serikali? Serikali iko wapi katika hilo, je wakulima wako tayari kuambiwa na jamii hiyo kuondoka wakaelewa, je ni jukumu la wafugaji kufanya hayo wanayofanya sasa ama jukumu la Serikali?

Ndungu zangu haya yote yanahitaji mtu mzalendo katika kushughulikia haya, kwakuwa naiamini Serikali ya awami ya tano ya Rais John Pombe Magufuli, chini ya wateule wake wa ngazi zote, sasa ni wakati wa kila mmoja wetu kuonyesha jitihada za kupunguza kama sio kuondoa tatizo hili

Uongozi wa Manyara chini ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dr Joel Nkaya Bendera, wakiwa na majibu ya maswali haya, migogoro ya wakulima na wafugaji Kiteto itakwisha, lakini kama hayatapatikana..wilaya ya kiteto itaendelea kubadilisha viongozi kila kukicha, kwa kuambiwa hawafai kwa kutoshuhulikia matamko ya viongozi hao

Mwanzo wa mgogoro wa ardhi kiteto, miaka minne iliyopita  nilishuhudia watu wakiletwa hospitali makundi kwa makundi eti wanapigana tena wakipigania ardhi, wakulima na wafugaji, wakiwa mashambani, hali iliyofanya Wilaya ya Kiteto kuitwa majina mengi mabaya kama Cosovo, Darfur na Somalia

Hali hii ilisababishwa na matamko ambapo yaliweza kuleta madhara, na kama Serikali wakati huo ingeweza kuchukua hatua haraka kukemea kauli hiyo hayo yote yasingejitokeza tena kwa kushughudia watu wakipoteza maisha

Yaliyojitokeza miaka hiyo iliyopita na kusababisha maafa, sasa yameanza kujitokeza baada ya kuanza kutolewa matamko kutoka kwa viongozi wa mila wa jamii ya kimasai, ambapo sasa wamedai tena hawataendelea kuvumilia uharibifu wa mazingira ukijitokeza Kiteto

Mwishoni mwa mwezi uliopita Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mhandisi Zephania Chaula, ambaye alikuwa kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, aliagizwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dr. Joel Nkaya Bendera kwenda kusikiliza malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha Partimbo kata ya Partimbo

Awali viongozi hao walienda kulalamika kwa Mkuu huyo wa Mkoa, kuhusu tamko la kamati ya ulinzi na usalama ya Kiteto walilotoa Nev 28 mwaka huu, kuwataka wananchi wa Kitongoji cha Njaniodo kijiji cha Partimbo, kuendelea na shughuli za kilimo tofauti na matakwa ya viongozi  wa Kijiji

Malalamiko ya awali yalikuwa wananchi hao wapatao 1561 wa kitongoji cha Njaniodo waliokuwa wanajishughulisha na kilimo na ufugaji, walitakiwa kuondoka katika eneo hilo kwa madai kuwa wako katika eneo la hifadhi

Kauli hiyo ilipingwa na wananchi hao na kwenda kulalamika kwa uongozi wa Wilaya ambao walitoa tamko la kuwataka kuendelea na shughuli zao, lakini uongozi wa Kijiji  nao walipinga na kwenda kulalamika mkoani ambapo, Mkuu wa

Mkoa alimwagiza mkuu wa Wilaya Mhandisi Zephania Chaula wa Simanjiro ambaye naye aliwataka kuendelea na kazi zao za kila siku kilimo na ufugaji wakati mpango wa matumizi bora ukiandaliwa

Maamuzi hayo yalipingwa tena na uongozi wa Kijiji cha Partimbo ambao walijitokeza kwenye chombo kimoja cha habari cha ITV kwa kutumia viongozi wa mila wakidai hawakubaliani na  kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Kiteto, kuwataka wananchi hao kuendelea na kazi za kibinadamu katika eneo walilodai la Ndirangoo

Katika matamshi hayo wako waliosema, kamwe hawakubaliani na tamko la Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, wengine wataenda hadi kwa Waziri wa ardhi William Lukuvi, wengine watahakikisha wakulima wa kitongoji cha Njaniodo hawatalima mwaka huu katika eneo la Ndirangoo

Wakati kukiwa na mvutano huo, Serikali ya Kiteto iliagiza kuwa kwa kuwa eneo hilo halikuwa katika mpango wa matumizi bora ya ardhi kijiji  kishirikishe wananchi wote, waanze kupanga matumizi bora ya ardhi jambo ambalo liliridhiwa na diwani wa kata ya Partimbo Mhe. Paulo Tunyoni

Kana kwamba haitoshi badala ya kuanza kutekeleza ushauri huo, matamko ya kuhatarisha amani Kiteto, yameanza kutolewa na waliojiita kuwa ni viongozi wa mila wa jamii ya kimasai kuwa hawakubaliani na maamuzi ya kamati ya ulinzi na usalama huku wakitishia wakulima kutofanya shughuli za kilimo katika maeneo hayo

Mvutano huu ni hatari sana, kuna kila sababu ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, kuonyesha utawala wake katika mkoa wake, awahakikishie wananchi,wakulima na wafugaji, usalama wao juu ya kauli hatarishi kama hizo, kwani awali ilitoka kama hivi baada ya kupuuzwa umma ulishuhudia maafa ya zaidi ya watu 30 huku kukiwa hakuna aliyetiwa hatiani

Na sasa matamko haya yameanza kutolewa ikiwa ni kipindi cha wakulima kutaka kuanza shughuli za kilimo, Serikali ya Kiteto inasema wakulima na wafugaji  wa Kitongoji cha Njaniodo wafanye kazi, Serikali ya kijiji inakataa kwa kutumia viongozi wa mila kuwa hawatokubali kuwaona wakulima katika maeneo hayo

Nionavyo,.. ubabe huu unaweza kuleta madhara kwa amani kuvunjika, kuna kila sababu ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dr. Joel Nkaya Bendera, kuvaa viatu vyake, kwani naamini vinamtosha, akiamua haya yanayoendelea kujitokeza Kiteto hayatatokea, na wananchi wako, wakulima na wafugaji wataheshimiana

Mwisho.

Maoni