Taso Kiteto walaami mkulima kuchomwa mkuki..


MWENYEKITI wa (TASO), chama cha wakulima na wafugaji, wilayani Kiteto mkoani Manyara, Bakari Maunganya, amelaani kitendo cha kujeruhiwa mkulima wa Kilosa akiwa shambani kwa kuchomwa mkuki mdomoni na kutokea shingoni, akisema huo ni ukatili unaopaswa kuitwa janga la Kitaifa

Migogoro ya wakulima na wafugaji imechangia vifo vingi na majeruhi hapa nchini, hivyo Serikali inapaswa kuliona kuwa hilo ni janga la Kitaifa kama yalivyo majanga mengine ambayo hushughulikiwa mara moja na kwisha

Akizungumza na MTANZANIA mwenyekiti huyo amesema, pamoja na kuendelea kuundwa tume kadhaa zikiwemo zile za kibunge, kamati mbalimbali, kuchunguza kiini halisi cha migogoro hiyo bado imekuwa tishio la maisha ya wakulima na wafugaji, huku Serikali ikiendelea kuunda tume hizo tena bila mafanikio

Alisema migogoro ya ardhi hapa nchini ni ya muda mrefu, ambayo imesababisha watu wengi kupoteza maisha, nafasi ya Serikali  ilikuwa ni kuhakikisha makundi hayo yanaishi kwa amani kwa kutumia sera na sheria zilizopo, badala yake, inaonekana kutokuwa na manufaa kwa makundi hayo

Naye Ramadhani Konki (mkulima) wilayani Kiteto alisema makundi ya wakulima na wafugaji yanaonekana kutelekezwa na Serikali  kwa kukosa mwongozo thabiti wa namna ya kufanya shughuli zao kwa uhakika ambapo ameiomba Serikali kuona haja ya kuwa na mpango kabambe wa kutatua migogoro hiyo

“ Kupanga matumizi bora ya ardhi inatakiwa kuendana na elimu kwa makundi hayo, hivyo kitendo cha Serikali kutokuwa wazi katika elimu hiyo, kumechangia kuendelea kujitokeza migogoro hiyo na kusababisha madhara makubwa kwa jamii”

Naye Ismail Sima (Mkulima) wa Kiteto alisema, Serikali haiwezi kuwepa lawama kwa kuchangia migogoro ya wakulima na wafugaji kutokana na kwamba wao ndio wenye mamlaka makubwa waliyopewa na wananchi ya kusimamia sheria

Zaidi ya watu 30 waliopoteza maisha Wilayani Kiteto mkoani Manyara, na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa kutokana na migogoro hiyo na hakuna mtu aliyetiwa hatiani kwa maafa hayo huku ikidaiwa kuna Serikali inayolinda raia na mali zao,alisema Sima

Kwa upande Omari Lumambo (mkulima) alisema migogoro ya ardhi Kiteto imesababisha kifo cha mwanae aitwaye Mhina Mndaira (29) ambapo ameitaka Serikali ya Kiteto kuona haja ya kumsaka mhalifu na kumfikisha mahakama kama ilivyo sheria za nchi hii

Kwa upande wake Lemomo Moringe kiongozi wa mila jamii ya kifugaji kijiji cha Ilela kata ya Partimbo alisema, tatizo la migogoro ya ardhi hasa kiteto linasababishwa na wakulima kuharibu mazingira kwa kukata miti hovyo, na kufanya kuwepo jangwa huku wafugaji wakihofu kukosa malisho ya mifugo yao

Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magesa, akizungumza na wananchi wa mji wa Kibaya aliwataka watu wenye ushahidi wa waliouawa waende polisi kufungua kesi upya ili uchunguzi wa vifo hivyo uanze mara moja kwani jambo hilo limeendelea kurudiwa na wananchi kila mara

“Wenye ushahidi wa maafa yaliyojitokea hapa Kiteto nendeni mkafungue kesi, sisi Serikali tutawasaidia nimemwambia OCD wangu hapa kuwa kuna haja ya kupokea lalamiko hilo upya la wananchi juu ya maafa haya kwani limekuwa likizungumzwa kila mara”alisema (DC) Magesa

MWISHO

Maoni