Tuwe na utamaduni wa kuandika vitabu.


Mkurugenzi mtendaji wa Halamshauri ya Wilaya ya Kiteto, Tamimu Kambona, Katika Uzinduzi wa Kitabu cha Kwanini Niko Hapa?uliofanyika jengo la maendeleo Kiteto..
                                       Uzinduzi wa Kitabu cha KWANINI NIKO HAPA?
Na MOHAMED HAMAD
UANDISHI wa vitabu, ni fani ambayo watu wengi wanaikwepa, kutokana na sababu mbamimbali, zikiwemo gharama, utashi wa mtu mwenyewe pamoja na kutokuwa na uelea wa kutosha juu ya uandishi wa vitabu.


Hali hiyo imefanya watu wengi kushindwa kuandika vitabu, na kujikuta wakiachia fursa hiyo adhimu, ambayo kwa hali ya kawaida mtu msomi, hapo ndio mahali pekee pakuonyesha uwezo wake kuhusu  kuandika vitabu.

Waliofanikiwa kuandika vitabu, kama vile Kitabu cha Ngugi wa Thiong’o, The river between, Things Fall Apart, walijipatia umaarufu mkubwa kwa kusomwa vitabu hivyo, huku vikitumika kama sehemu ya masomo ya fasihi katika shule za Sekondari na vyuo

Kule Nigeria,.. kuna mwaandishi maarufu, Profesa Wole Soyinka, aliyekuwa ameandika vitabu kama vile Death and the King’s Horseman, hawa wamejipatia umaarufu mkubwa hapa duniani si tu kuandika vitabu bali waliweza kutimiza wajibu wao

Hatuna budi kuwaunga mkono waandishi hawa wa vitabu na kuwataka kujitokeza kwa wingi kuandika vitabu zaidi ili viweze kusomwa na kuleta mabadiliko ndani ya jamii kwa kuelimisha, kuburudisha, kuadabisha na kuhifadhi amali za jamii husika

Pamoja na kuwepo tabia za watu wengi kutokuwa na utamaduni wa kusoma vitabu, vitabu hivyo vimekuwa na manufaa makubwa kwa baadhi ya watu ambao, wanaendelea kunufaika navyo kwa kutumia muda wao kuvisoma na kubadilisha maisha yao

Katika kuunga mkono jitihada hizo, kijana Samwel E.Maphie, mkazi wa Kiteto mkoani Manyara, aliyezaliwa mwaka 1988, ameandika kitabu chenye jina la KWANINI NIKO HAPA? Kikiwa na mambo nane ya namna ya kumfanya mtu atoke katika hali ya kukata tamaa .

Kwa mujibu wa mtunzi wa kitabu hicho alisema, alizunguka katika uso wa Dunia na kuona watu wengi wakiwa wamekata tamaa, wakati wengine wakilia wengine wanacheka, wakati wengine wakiangamia wengine wananufaika na maangamizi hayo.

Alisema kitabu cha KWANINI NIKO HAPA? Ni jibu la matatizo hayo, kwani kimeonyesha namna mtu anavyoweza kukabiliana na aina yoyote ya changamoto aliyonayo, mkubwa kwa mdogo, hasa akitaka kila mtu kujiona kuwa ana sababu ya kuwepo hapa duniani.

Anasema kwa hali ilivyo sasa, kuna mamilioni ya watu wamepoteza mfumo wa maisha yao halisi, wanaishi kuholela bila kuwa na malengo, huku wakitaabika bila kujua cha kufanya na hata wengine kuamua kufanya maamuzi magumu ya kukatisha maisha yao.

Alisema maisha hayo sio mpango wa Mungu bali ni mipango ya baadhi ya watu ambao wameamua kuwangamiza, akisema  kuna kila sababu ya kupitia malengo hayo nane ndani ya kitabu hicho ambayo ndio jibu sahihi la maisha haya

"Kwa sasa tunaona maisha ya watu wengi yakiteketea kwa vita,majanga,na hata kudhalilika mitaani kutokana na mipango hiyo ya kibinadamu ambayo imejengwa kwa misingi ya kunufaika kwa baadhi ya watu wanapopata matatizo hayo” alisema mtunzi huyo akiwa katika hali ya huzuni wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Tamimu Kambona, katika uzinduzi wa kitabu hicho alisema, mtunzi wa Kitabu cha KWANINI NIKO HAPA?  Ni lulu na faraja ya Kiteto, ambapo kwa sasa wananchi wengi wanaonekana kukata tamaa kutokana na migogoro ya ardhi.

Alisema toka ameteuliwa kushina nafasi hiyo, amekuwa akishughulika na utatuzi wa migogoro ya ardhi ambayo hadi sasa haijaisha, akisema Kitabu cha KWANINI NIKO HAPA? Kitakuwa msaada kwa wananchi hao na wengine wote wenye matatizo yanayowakabili katika maisha yao.

Katika hatua hiyo, Kambona aliwataka vijana wasomi Wilayani Kiteto, kutumia elimu zao kusaidia jamii kutatua migogoro hiyo na kuwalaani wale wanaoitumia kama vyanzo vya mapato yao ili hali wakijua wananchi wanapata madhara yakiwemo vifo, kupoteza maisha na hata kupata vilema vya kudumu.

“Nitaendelea kuwaunga mkono vijana kama hawa, Ndugu Samweli, wewe ni lulu ya Kiteto…,Ndugu Samweli, wewe ni mwanga wa Kiteto..,tumwombe Mungu akulinde ili uendelee kusaidia Kiteto na Taifa kwa ujumla” alisema Mkurugenzi huyo huku akionekana kuvutiwa na kazi ya uandishi wa kitabu hicho

Kwa upande wake Patrick Kimaro (Sabasita) Mkuu wa Polisi Kiteto, akiwa katika uzinduzi huo wa kitabu alisema, kitabu hicho kitapunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa kama kitasomwa na wananchi waliowengi,
Alisema uhalifu unaongezeka siku hadi siku kufuatia sababu mbalimbali, na kuwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kusoma vitabu, sambamba na kujiongeza katika kufuatilia mambo yanayowahusu  ya kila siku

Naye mwenyekiti wa maandalizi ya uzinduzi wa kitabu hicho, Nason Kikando, alimtaka mtunzi wa kitabu hicho Samwel Maphie, kuhakikisha kuwa anakisambaza vya kutosha ndani ya jamii ili waweze kukisoma kwa lengo la kufikia matarajio yake ambayo ni kuona Taifa likiishi kwa amani bila uonevu


“Najua dhamira halisi ya mwandishi wa kitabu hiki, ni baada ya kuona watu wakitaabika kwa matatizo mbalimbali yanayofanya wakate tamaa, sasa kitabu hiki kiwafikie kwa wingi ili waweze kukisoma na mwisho wa siku wabadilike”alisema Mwenyekiti huyo

Jumla ya nakala 1,000 za kitabu cha kwanini niko hapa? zimeanza kutawanywa kwa kuuzwa katika mikoa ya Manyara na Arusha, ambapo imeelezwa kuwa zitakuwa msaada mkubwa katika ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili wananchi yakiwemo migogoro ya ardhi pamoja na kujiimarisha kiuchumi

Pia kwa mujibu wa mtunzi wa kitabu hicho alisema katika uzinduzi wa kitabu hicho 40% za mauzo zitapelekwa hospitali ya Wilaya ya Kiteto kwaajili ya kuchangia sekta ya afya kutokana na changamoto zilizopo

Kwa mujibu wa baadhi ya vijana na wazee walioweza kusoma kitabu hicho walisema, Kitabu hicho ni lulu ba silaha ya Kiteto ambayo watawala wakiitumia waanaweza kuondokana na changamoto zilizopo, ambapo hadi sasa Wilaya imedaiwa kuwa na changamoto nyingi zikiwemo migogoro ya ardhi pamoja na kutopatikana huduma za jamii kwa kiwango stahili

Mwisho

Maoni