Kiteto na changamoto za maendeleo..



                                                                   Tatizo la maji Kiteto..
                                           Uhaba wa madarasa shule za msingi Kiteto...




Na, MOHAMED HAMAD
WILAYA ya Kiteto ilizinduliwa mwaka 1974, ina ukubwa wa km za mraba elfu 16.6, mgawanyo wa matumizi bora ya ardhi kilimo ni hekta 3800 sawa 23.4%, huku eneo la hifadhi na malisho pamoja na uwindaji ikiwa hekta 11,111 sawa na 66.6%
 
Msitu wa asili ni hekta 1,089.6 sawa 10% ambapo kwa mujibu wa idadi ya sense ya watu na makazi ya mwaka 2012, wilaya ina jumla ya watu 254,669, sawa na 80% ya wakulima  na wafugaji,  20% wakijihusisha na biashara ndogondogo.
 
Wilaya ina hifadhi ya Emboley Murtangos mbayo eneo lake limetolewa na vijiji saba Partimbo hekta 48,557.79, Namelock hekta 35,082.72,Lortepes hekta 34,974.79,Nhati 2,846.85, Emart hekta 1,630.97,Egusero Sidani 2,692.87, Ndirigish hekta 7,553.16, jumla ya eneo lote ni hekta 133,333.15.
 
Wilaya ya Kiteto ina migogoro ya ardhi, ndani na mipaka na Wilaya za jirani, mbali na mgogoro mama wa wakulima na wafugaji ambao ulianza toka mwaka 2012, uliofanya baadhi ya watu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa wakigombea ardhi
 
Baadhi ya wakulima walishtaki halmashauri ya wilaya kwa kuwaondoa shambani kwa nguvu, na kushinda kesi iliyoamuru halmashauri kulipa fidia ya bil 1.2 kisha halmashauri kukata rufaa na kuamriwa kutotakiwa wakulima na wafugaji katika eneo hilo la Emboley Murtangos kufanya shughuli za kibinadamu.
 
Maamuzi hayo hayakuweza kuheshimiwa na makundi hayo ambapo kila kundi lilijiona kuwa na haki ya kutumia eneo hilo, ambapo wafugaji waliingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima kisha kuwapiga wakidai kulima maeneo ya malisho
 
Hali hiyo iliibua mgogoro kati ya makundi hayo na kusababisha  maafa zaidi ya watu 30 na wengine 200 kujeruhiwa kwa kugombea ardhi, hali ambayo ilisukuma uongozi wa ngazi ya juu kuingilia kati kunusuru hali hiyo
 
Serikali iliunda tume pamoja na kamati mbalimbali kunusuru maafa hayo sambamba na kufanya mabadiliko ya kiutawala kwa viongozi wa halmashauri ya hiyo hali inayodaiwa kuleta matumaini ya kurejea kwa amani.
Tatizo la maji
 
Wilaya ya Kiteto inauwezo wa kuhudumia wananchi wake wa vijijini maji safi na salama kwa 36, huku kwa upande wa mijini  37% hali inayofanya wananchi kutumia muda mwingi kusaka maji kuliko kufanya shughuli zingine za maendeleo.
 
Hali hiyo imedaiwa kuwachelewesha wananchi kimaendeleo toka wilaya izinduliwe mwaka 1974 ikiwa na watu 12,000, wameongezeka na kufikia zaidi ya laki mbili, huku ikiendelea kutumia miundimbinu ya maji ya zamani.
 
Kijiji cha Sunya wilayani Kiteto mkoani Manyara, chenye wakaazi 12,000, hakina chanzo cha maji ya kisima kirefu kilichochimbwa wala bwawa hali inayowalazimu kutumia maji ambayo sio safi na salama kutoka kwenye makorongo
 
Kata ya Kijungu wilayani humo, wananchi wanalazimika kutumia zaidi ya masaa nane kusaka maji kwa kutembea umbali mrefu na kusababisha washindwe kufanya shughuli zingine za maendeleo kutokana na uhaba wa maji.
Miundombinu ya barabara
 
Miundombinu ya barabara wilayani Kiteto imetajwa kuchangia kutofikiwa malengo ya wananchi tarajiwa kwa wakati, kutokana na baadhi ya maeneo kutofikika kwa usafiri wa barabara kutokana na ubovu wa miundombinu hiyo.
 
Wananchi wa kata ya Dongo wilayani Kiteto, wakitaka kufika makao makuu ya wilaya wanalazimika kupitia eneo la wilaya nyungine Pandambili iliyopo Kongwa ambako ni rahisi kufika kwa magari kisha kuanza safari kwenda makao makuu ya wilaya ya Kiteto iliyopo Kibaya.
Afya
 
Kata ya Partimbo ni moja kati ya kata wilayani Kiteto ambayo haina zahatati wala kituo cha afya, hali inayofanya wananchi kutumia gharama kubwa kwenda hospitali kusaka huduma ya afya.
 
Taarifa za uhakika zinaeleza wananchi wa kata hiyo wanalazimika kutumia madawa ya asili na ikishindikana ndio wanakwenda hospitali ya wilaya ya Kiteto tena wakiwa wamechelewa kupatiwa matibabu.
 
“ Huwezi kuamini wengi wa wananchi wa kata ya Patimbo ni wafugaji..wanapoteza maisha kwa kuchelewa kufika hospitali baada ya kushindwa jaribio la kutibu wagonjwa wao kiasili na wakati mwingine hupoteza maisha utokuwa a Zahanati” alisema Paulo Tunyoni diwani wa kata hiyo.
Elimu.
 
Baadhi ya vijiji wilayani kiteto, vimetajwa kutokuwa na shule za msingi, na kutakiwa wilaya kuona haja ya kuingilia kati ili kuwawezesha kizazi hicho kupata elimu kama yalivyo maeneo mengine.
Vijiji vinavyodaiwa kutokuwa na shule  huku idadi kubwa ya wanafunzi wakikosa haki ya kikatiba ya kupata elimu ni pamoja na Ngabolo, Ngapapa, na Lerug, vyoye vilivyopo wilayani Kiteto.
 
Baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo wamesema, serikali inaonekana kutoona umuhimu wa kusogeza huduma hiyo karibu na wao, jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi hii na kuwaomba sasa kuona umuhimu huo.
 
“Haingii akilini Tanzania kusikia baadhi ya vijiji havija  shule za msingi, achilia mbali sekondari, tunaomba Serikali ya Kiteto wakumbuke hata wananchi wa maeneo Ngabolo tunataka shule” alisema Mohamed Iddi (mwananchi)
Kauli ya Mbunge
 
Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Emmanuel Papian, katika maeneo tofauti mbele ya wananchi pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali wilayani hapo, alisema suala la amani itarejea endapo taarifa za tume zilizoundwa  na aliyekuwa Waziri mkuu Mizengo Pinda zitafikishwa kwa wananchi
 
Alisema kwa miaka mitano sasa maafa ya wakulima na wafugaji yaliyotokana na mapigano ya kugombea ardhi hayajatokea tofauti na miaka iliyopita kutokana na wananchi kuahirishiwa matatizo yao na viongozi wao.
 
Kila kiongozi aliyefika na kuelezwa matatizo ya wananchi Kiteto alisema, wananchi wawe na subra Waziri Mkuu Kassimu Kassimu Majaliwa atafika kuja kutatua, huku wakiendelea kusubiri utatuzi huo.
 
“Nilipokea Jimbo likiwa na manug’uniko makubwa ya wananchi kutokana na dhulma, rushwa, ubaguzi, ukabila, pamoja na kutowajibika kwa baadhi ya viongozi wa Serikali kwa maksudi, hali iliyosababisha madhara kwa wananchi kama maafa na majeruhi”alisema Papian.
 
Kiteto inakabiliwa na tatizo la maji,afya,elimu na miundombinu,katika kuhakikisha matatizo hayo yanapungua kama sio kwisha nipo bega kwa bega viongozi wenzangu kama madiwani na wakuu wa idara, katika kupanga bajeti na kuisimamia.
 
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, ambaye ni mwenyekiti wa ulinzi na usalama wa Wilaya pamoja na wajumbe wake wamekuwa msaada mkubwa kuhakikisha amani inatawala kwa kutoa nafasi kwa 
wananchi kufanya kazi
 
“Ni kweli halmashauri ya wilaya ina uwezo wa kuhudumia wananchi wake kwa asilimia 48% tu,  eneo la vijijini ni 36% na mjini 37%, hali inayofanya wananchi washindwe kufanya shughuli zingine za  maendeleo, jitihada zinaendelea kwa wahisani Wamisri kuchimba visima virefu tukishirikiana na Wizara ya maji na umwagiliaji.
 
Sekta ya elimu, Kiteto inakabiliwa na changamoto za uhaba wa madarasa, waalimu wa sayansi, ambapo hadi hivi sasa kuna shule za msingi 90 zenye wanafunzi wanaokadiriwa kuwa kati ya elfu 35-36 huku idadi ya shule za sekondari zikiwa 16 zenye wanafunzi elfu nne.
 
Mbunge Papiani alikiri baadhi ya vijiji kutokuwa na shule akidai jitihada zipo hata wananchi wenyewe wanaona Serikali yao ya awamu ya tano ilivyo macho ikitazama kila kona, na tatizo barabara kwa baadhi ya maeneo nalo linashughulikiwa
 
Alisema amelifikisha malalamiko kwa wahusika, na Suala la afya nalo lipo katika mipango ya 
Serikali ingawa bajeti ya mwaka 2016-2017 na 2017-2018 imelenga kumaliza viporo vya miradi ya ambayo haikumalizima.
 
mwisho

Maoni