RC Manyara atoa siku 7 wanafunzi watoro kurejea shule.

Mkuu wa mkoa wa Manyara, DR. Joel Nkaya Bendera..


Na, MOHAMED HAMAD, KITETO.
MKUU wa mkoa wa Manyara, Dr. Joel Nkaya Bendera, ametoa siku saba kwa
wanafunzi watoro mkoani humo, kurejea shuleni kabla hatua kali za
kisheria hazijaanza kuchukuliwa ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Dr. Bendera ameyasema hayo juzi wakati akizungumza na mamia ya
wananchi wa kijiji cha Kijungu, Wilayani Kiteto kufuatia taarifa ya
wanafunzi wengi waliofaulu kutojiunga na kidato cha kwanza kutokana na
sababu mbalimbali.

Alisema Taifa lisilokuwa na wasomi haliwezi kuendelea, akidai matokeo
ya mtihani wa Taifa mwaka huu mkoani Manyara yanaonyesha kumeshuka
kielimu kwa kushika nafasi  ya 20 Kitaifa na kuwataka wananchi kwa
ujumla kuona umuhimu wa elimu katika mkoa huo.

“Nimepewa dhamana ya kuongoza Mkoa huu wa Maanyara kimaendeleo,
sitakubali kuona hali hii ikiendelea,  nitoa siku saba watoto kuripoti
shule wale wote ambao hawakufika, natoa wito kwa wenyeviti wa vijiji,
watendaji, makatibu Tarafa, Mkurugenzi uko hapa na wewe mkuu wa Wilaya
hakikisha wanafunzi hao wanafika shuleni” alisema Dr. Bendera.

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magessa, alimweleza mkuu huyo wa
Mkoa kuwa idadi kubwa ya wanafunzi waliofaulu kuingia kidato cha
kwanza, hawakuripoti kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo mimba na
utoro unaochangiwa na wazazi na walezi.

“Mhe Mkuu wa Mkoa, hapa Kijungu Sekondari nimepata taarifa ya
wanafunzi 11 waliofaulu hawakuripoti shule, Wilaya tuna mkakati wa
kuhakikisha wanafunzi hao wanaripoti ili waweze kuendelea na masomo
yao, ikizingatiwa Serikali ya awamu ya tano inasisitiza kila motto
kwenda shule” alisema.

Akizungumzia utoro huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Kiteto, Tamimu Kambona, alisema utoro huo umetokana na baadhi ya
wazazi na walezi kutokuwa na mwamko wa elimu, kuwatumia watoto kama
vyanzo vya mapato kuchunga mifugo na kuolewa.

Alisema watoto wa kiume kwa jamii ya kifugaji wanalazimishwa kuchunga
mifugo, huku wakike wakiolewa hata kama wamepata bahati ya kuendelea
na masomo, hivyo huhamahama na mifugo jambo linalofanya kazi ya
kuwasaka kuwa ngumu wanapozurura na mifugo.

Kwa upande wa baadhi ya wanafunzi kutoka jamii ya kifugaji wilayani
kiteto, wamekiri kutumikishwa na wazazi wao kuchunga mifugo na hata
kuolewa na kukatishwa masomo na kuitaka Serikali kuingilia kati kupiga
vita tabia hiyo ambayo inawanyima haki ya masomo

Mwisho.

Maoni