Barua ya wastaafu kwa mh. Rais

                                                                      Picha juu ni
                                                     Rais Dr. John Pombe Magufuli..

                                                                 R.A. Mhina
                                                           MAJOR  MSTAAF

Ndugu mhariri
SERIKALI ya awamu ya tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, siku zote imekuwa kimbilio la wanyonge kama anavyosema katika mikutano yake kuwa, hataki kusikia wananchi wa Tanzania hasa maskini wakilia shida wakati kuna watumishi wa Serikali wanaolipwa fedha  kwaajili yao

Naamini kauli hii inatupa faraja tuliowengi, hasa mimi ambaye nimelazimika kuandia barua hii kwako,  nikilenga kuwa unauwezo na ni msikivu, mwepesi usikie kilio cha wastaafu wa zamani, ambao kwa sasa tunaishi kwa taabu kubwa kutokana na kipato kidogo tunachopata toka Serikalini

Ni ukweli usio pingika kuwa kwa sasa Watanzania wengi tunaishi chini ya dola moja, nikimaanisha kiasi hicho hakikidhi mahitaji ya mtu na familia kwa ujumla ikizingatiwa pia watumishi wastaafu wa zamani katika nchi hii wengi wetu tulijitoa muhanga kuitetea nchi hadi hapa ilipofikia

Kwa hali ya kawaida mtu mzima kupata 1666 kwa siku sawa na elfu hamsini (50,000) kwa mwezi, kiasi hiki hakitoshi, ikizingatiwa mtu huyo aliitumikia nchi hii mpaka sasa amechoka na hawezi kufanya kazi yenye kupatia kipato kikubwa

Kwa niaba ya wastaafu wenzangu, naomba Serikali ya awamu ya tano, ya Rais Dkt John Pombe Magufuli, kusikia kilio hiki ambacho kimegusa tawala zote lakini hakikutatuliwa hali inayosababisha wengi wetu kukata tamaa na kuishi kama watumwa ndani ya nchi yao

Ili kuonyesha kuwa taarifa hizi zimefika kwa walengwa kutaka kutatuliwa, wazee wastaafu wa nchi hii kwa nyakati tofauti tuliweza kuandika malalamiko yetu kwa Waziri wa Fedha toka mwaka 2010 na kuishia ahadi zisizotekelezwa.

Baadaye tulikutana na Rais Mstaafu, wa awamu ya nne Dr. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye aliweza kutoa maelekezo kwa Waziri wa fedha Saada Nkuya, lakini hakuna utekelezaji uliofanyika, ambapo sasa kwa Serikali hii naamini linawezekana

Katika mazungumzo hayo, pia tulimwomba Mh Rais aweze kulitazama suala la wajane wa wastaafu ambao waliishi kwa kutumia fedha hizo lakini wamekatiwa msaada huo kwakuwa waume zao wamefariki

Kitendo cha kukatwa msaada huo, kimewaathiri wajane hao kwa namna moja ama nyingine kwani waliishi kwa kutegemea pensheni za waume zao ambao waliishi nao enzi za uhai wao hivyo kwa busara yako Mh Rais, tunaomba uendelee kuwalipa hadi mwisho wa uhai wao

Jambo lingine ni kuhusu sherehe ya mashujaa.. Mhe Rais, sherehe hizi ni katika kuwakumbuka na kuwaenzi mashujaa waliopigania ukombozi wa kusini mwa Afrika na vita vya Kagera, hawa nao wametelekezwa kwa kutoshirikishwa katika sherehe hizo

Kutokana na umuhimu wa sherehe hizo, kuna kila sababu ya walengwa hao kushirikishwa kikamilifu japo kwa uwakilishi kwa kila wilaya kama ilivyo dhamira ya sherehe hiyo ambayo inaitika kama SHEREHE ZA MASHUJAA.

Mhe. Rais kwa niaba ya wastaafu wenzangu, tunaimani na Serikali ya awamu ya tano, ambayo mara zote imekuwa na huruma kwa wanyonge bila kujali itikadi za watu, hivyo tunaomba kilio hiki kipatiwe ufumbuzi ili kunusuru maisha ya wastaafu na wajane

Kwa niaba ya wasaafu wenzangu.
R.A. Mhina
MAJOR  MSTAAF

KITETO, MANYARA.TEL 0765583574.

Maoni