Ukeketaji Kiteto ni biashara kwa ngariba





 Na, MOHAMED HAMAD

SERIKALI Wilayani Kiteto mkoani Manyara imebaini kuwa, ukeketaji wa akinamama na watoto wa kike, umekuwa biashara kwa ngariba ambayo inawapatia kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku.

Akizungumza na MTANZANIA, Joseph Mwaleba, afisa maendeleo ya jamii wilayani Kiteto amesema, pamoja na jitihada za Serikali kukabiliana na tatizo hilo, bado mbinu zinazidi kuibuliwa na ngariba kufanikisha zoezi hilo

“Mbinu zinazotumika kufanikisha zoezi la ukeketaji ni kusafirisha watoto kwenda kwa ndugu, ama kukeketwa watoto mara wanapozaliwa, ili kutimiza adhma iliyokusudiwa na wahusika katika zoezi hilo”alisema Mwaleba

Baadhi ya akinamama walioacha kazi ya ukeketaji (mangariba)  ambao hawakutaka kutaja majina yao walisema, kitendo hicho hakina faida bali ni mazoea yaliyojengeka kwa baadhi ya makabila na hasa yakishinikizwa na baadhi yao

“Wanasema mwanamke ambaye hakukeketwa anaonekana ndani ya jamii kama mtoto mdogo, hawezi kusema mbele ya wenzao waliokeketwa, hivyo kinachotakiwa ili aweze kueleweka lazima akeketwe”walisema

Pia ujira wanaopata kwa shughuli za ukeketaji umetajwa kuwa sababu ya shinikizo la ukeketaji, na kusema kazi hiyo inawapa heshima ndani ya jamii na hata kipato katika maisha yao, alisema mmoja wa akinamama hao

Kwa upande wa baadhi ya wasichana waliofanyiwa vitendo hivyo walisema, ili kuzuia ukeketaji mbali na kukamata wahusika kuna kila sababu ya kuwapa mikopo akinamama hao waliozoea biashara hiyo kuachana na biashara hizo haramu

Wametaja baadhi ya madhara yanayotokana na ukeketaji kuwa ni pamoja na kutokwa na damu nyingi hadi kupoteza maisha, kupata kilema cha kudumu, pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kuondolewa kiungo cha mwili bila ridha yao

mwisho

Maoni