Wafugaji Kiteto ni aibu kunyima watoto wenu elimu

.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto DC Tumaini Magessa akiwa katika mkakati wa kuwawezesha wafugaji kupata elimu.


Na, MOHAMED HAMAD
WILAYA ya Kiteto, ilisomeka kama eneo la wafugaji (maasai), wakati huo iliitwa masai land, hali iliyowaaminisha watu wengi kuwa, eneo hilo ni la jamii ya kifugaji wamasai, ingawa kuna makabila mengi mchanganyiko yanayojihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Nijuavyo mafanikio yoyote ya mwanadamu, elimu inachukua sehemu kubwa, pamoja na kwamba jamii hiyo ndio waasisi katika maeneo hayo, makabila mengine yameingia kwa kasi kubwa na kufanya mchanganyiko wa watu ambao sasa matabaka yanajitokeza

Makabila mengine hayo ni kama vile, warangi, wanguu, wachaga, wagogo na mengine mengi yamepokea kwa haraka sana suala la elimu, na kuamua kusomesha watoto wao tofauti na jamii ya kifugaji wamasai

Kinachoendelea sasa ni Serikali kuamua kukamata watoto wa jamii hiyo na kuawandikisha shule, ili waweze kupata haki yao ya kikatiba, jambo ambalo kwa karne hii mzazi haeleweki kwa kutopeleka shule mwanae

Kana kwamba hii haitoshi, jitihada za baadhi ya wazazi na walezi kwa jamii hiyo, ni kuhama na watoto hao kusiko julikana ili watoto hao wasiweze kupata haki yao ya kikatiba, ambapo Serikali nayo kwa kuona hivyo imeamua kuwakmata kwa nguvu na kuwaandikisha shule

Nijuavyo, lengo la Serikali ni jema kabisa na ndio wajibu wao kutoa elimu kwa wananchi wao, ila sio kwa kiwango cha kukamatana kwa nguvu kama ilivyo kwa jamii ya kifugaji wamasai wa Kiteto, kwa maeneo mengine hapa nchini huwezi kueleweka

Ili kuwa na usawa wa kikatiba kielimu, kuna kila sababu ya jamii ya kifugaji kubadilika tena kwa haraka tena kwa kuiga kutoka kwa makabila mengine, ambao elimu kwao ni jambo la kawaida kusomesha watoto wao bila shuruti

Ukienda baadhi ya mikoa hapa nchini, kama vile Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Mwanza na kwingineko, suala la elimu linafahamika kuwa ni jukumu la mzazi kuhakikisha kuwa anamuandaa mwanae kupata elimu ambayo Serikali imejipanga kutoa

Tofauti kabisa na Kiteto, tena kwa jamii moja ya kifugaji wamasai, wao Serikali inatumia nguvu kubwa kuwapa  elimu, huku wao wakipambana nayo kwa kubuni mbinu mbalimbali za kuwafanya watoto wao wasiende shule tena wakiwatumikisha kwa kuchunga mifugo

Kwa kawaida shughuli kuu za jamii ya kifugaji ni ufugaji  huria, ambapo mfugaji huonekana kuwa wa maana na thamani pale atakapokuwa na mifugo mingi, jambo ambalo kwa sasa halina tija kutokana na ongezeko la watu ambapo kila mara migogoro huibuka

Katika mashindano ya nani ana mifugo mingi hapa Kiteto, madhara makubwa ni kwa watoto wao kuntimwa elimu kwa kutoandikishwa shule, huku wakihamahama na mifugo, hali inayofanya wengi wao kukosa haki yao ya kikatiba

Kutokana na hali hiyo, Serikali wilayani Kiteto inaonekana kuvutana na wafugaji hao kutaka kuwapa elimu, lakini bado changamoto ni kubwa kwao na madhara zaidi yanajitokeza kwa jamii hiyo kushindwa kuendana na matakwa ya jamii na hata Serikali kwa ujumla inapotoa maelekezo, huchelea kuyapata

Ili mtu aweze kuendana na kinachotakiwa na Serikali, elimu ni jambo jema na kipaombele  cha kumfanya kupata uelewa wa haraka tena bila usubufu, kazi ambayo ndiyo inayoendelea kufanywa na Serikali zote hasa ya awamu ya tano ya Rais John Pombe Magufuli

Kwa sasa elimu imetajwa kuwa bure, kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule, anatakiwa kuandikishwa ili aweze kupatiwa elimu ya kumfanya aweze kumudu maisha yake na kujiletea maendeleo na Taifa lake kwa ujumla

Hongera Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, pamoja na uongozi wa halmashauri ya Kiteto kwa kuanzisha msako wa kusaka watoto ambao wazazi wao wamekaidi kuwaandikisha shule, kwani mafanikio yake unaweza kuyapima kwa muda mfupi sana baada ya watoto hao kumaliza shule

Jamii ya kifugaji badilikeni sasa tuko katika karne nyingine kabisa ambayo, wenzetu walishatoka huko zaidi ya miaka mingi iliyopita, tuachane na tabia za kuwatumia watoto kama wajakazi kuchunga mifugo na kuwaoza kama jukumu lao waliloumbiwa

Mwisho.

Maoni