Maagizo ya RC Mnyeti yasipuuzwe

Mkuu wa mkoa wa Manyara ALEXANDER MYETI akifafanua jambo mbele ya watumishi wa Serikali ambao hawapo pichani akiwa Kiteto Manyara Tanzania..


NA MOHAMED HAMAD MANYARA.

NIMPONGEZE Mkuu wa mkoa wa manyara Alexander Mnyeti, kwa kuonyesha msimamo wake katika kuwatumikia wananchi katika mkoa huo kwa uadilifu na kuwataka kila mmoja awajibike katika nafasi yake.

Maagizo haya ni ya kiutendaji zaidi na yanayoendana na kasi ya Rais Dr. John Pombe Magufuli, ambaye kila mara ameonekana kutanguliza maslahi ya umma mbele.

Alexander Mnyeti ni Mkuu mpya wa Manyara, aliyeteuliwa miezi miwili iliyopita, akitokea Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha akiwa kama mkuu wa Wilaya, na huu ni mkoa wake wa kwanza kuongoza.

Kwa hali isiyofichika mkoa wa Manyara una changamoto nyingi za kimaendeleo zinazosababishwa na baadhi ya viongozi wa Kiserikali na Kisiasa, kuvutana kutaka kuonyeshana umwamba huku wananchi wakitaabika.

Hali hii imewachelewesha wananchi kimaendeleo na kufanya kulalamika kila kukicha wanapokutana na viongozi wa ngazi za juu huku wakiahidiwa kutatuliwa kero zao miaka nenda miaka rudi bila mafanikio ya kudumu.

Akiwa ziarani Kiteto mkoani humo Mkuu huyo wa mkoa wa Manyara, ameonyesha uwezo wake wa kupokea changamoto za wananchi na kuzitafutia majibu ya haraka jambo ambalo limewapa faraja wananchi waliokuwa wameanza kukata tama kuwa hahawezi kusaidika.

Mkuu huyo wa mkoa mbali na ukaguzi alioufanya katika miradi ya maendeleo ujenzi na kutoa maelekezo ya Serikali, pia amefanya mikutano mitano ya wananchi katika maeneo tofauti wilayani humo.

Mikutano hiyo ilitawaliwa na malalamiko yaliyohusu migogoro ya ardhi kwa zaidi ya 75% huku huduma za elimu, afya, maji  na miundombinu ya barabara ikipata asilimia zilizobakia katika kulalamikiwa.

Hali hii imempa ujasiri mkubwa Mkuu huyo wa mkoa kuchukua hatua kwa baadhi ya watumishi wa Serikali na kupendekeza njia bora kwa watumishi wengine waliobaki katika kuwatumikia vyema wananchi.

Pia aliwakemea baadhi ya wanasiasa aliowaita chanzo cha migogoro hiyo na kumwagiza mkuu wa Wilaya ya Kiteto Tumaini Magesa kuwakamata itakapobainika kuhatarisha amani ili hatua za sheria zifuate.

Kuhusu watumishi wa Serikali aliwaambia kuwa kama kuna mtumishi yoyote hatoweza kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano atoe nafasi kabla hajafikiwa na maamuzi mazito huku akiwaasa kuwa mwananchi ndio mwajiri wao.

Ziara hiyo ilitawaliwa na maagizo ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Tumaini Magesa, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya Tamimu Kambona na Mkuu wa Polisi Kiteto Fadhili Luoga kuwa wakitekeleza wajibu wao wananchi watabaki salama.

Maagizo hayo yalienda sambamba na muda wa utekelezaji wake ambapo kila walipopewa walikubaliana muda wa utekelezaji jambo ambalo limedaiwa kuwa halijapata kutokea kwa viongozi wa siku za hivi karibuni.

Mkuu huyo wa Mkoa alimaliza ziara yake akiahidi kurejea baada ya miezi minne wilayani humo kutaka kuona utekelezaji wake huku akiapa kuwa yeye sio Mkuu wa mkoa wa maboksi ambayo mvua ikinyesha yatalowana.

Nimalizie kwa kusema nawatakiwa utekelezaji wa maagizo mema viongozi wa Kiteto na Mkoa wa Manyara kwa ujumla yaliyotolewa na mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti na kwa wale wengine nao wajipime kama wanaweza kuendana na kasi yake..

Mwisho.


Maoni