Jitihada za viongozi Kiteto ni za kuigwa.

Jengo la kituo cha afya Sunya linalopanuliwa na kujengwa majengo mapya matano ya kisasa..


Jitihada za viongozi Kiteto ni za kuigwa.

NA. MOHAMED HAMAD.
Miradi ya maendeleo wilayani Kiteto mkoani Manyara, imetajwa kuwa kivutio cha viongozi hapa nchini, kutokana na usimamizi wa majengo hayo.

Miongoni mwa viongozi waliovutiwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemaji Jafo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti na viongozi wengine wengi mkoani Manyara.

Kituo cha Afya Sunya, kimekuwa kivutio ambacho serikali ilitoa mil 400 kujenga majengo matano, jengo la ofisi za Serikali la thamani ya bil 4.3 linaloendelea kujengwa.

Mengine ni majengo ya sekondari ya Engusero iliyopandishwa hadi kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita wilayani humo.

Serikali ilitoa fedha kwaajili ya miradi hiyo baada ya kuonekana uhitaji wa huduma hizo, kisha kutoa maelekezo ya namna ya kutekeleza ili ilete tija kwa jamii.
Kwa nyakati tofauti viongozi hao, wamekuwa wakitembelea miradi hiyo na kujiridhisha namna inavyotekelezwa kulingana na fedha zilizotolewa na Serikali.

Waziri Jafo alisema baada ya kukamilika majengo ya kituo cha Afya Sunya ataleta vifaa tiba pamoja na madawa ya mil 300 ili huduma ya afya iweze kutolewa kwa wananchi.

Kituo hicho kina vyumba maalumu vya wajawazito kujifungulia  mbali na vilivyopo hapa nchini katika hospitali ya Taifa muhimbili ambapo katika maeneo ya wilayani kata pekee iliyobahatika kujengewa vyumba hivyo ni Sunya.

Majengo mengine ni ofisi za Serikali ghorofa moja zinazoendelea kujengwa kwa gharama ya bil 4.3 mjini Kibaya kuwa ni mfano wa kuigwa katika maeneo mengine hapa nchini.

Hata hivyo mfumo unaotumika wa ujenzi huo ni kutumia mafundi wa kawaida (Force account) ambapo msimamizi wa miradi hiyo ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Bw. Tamimu Kambona.

Katika kufanikisha ujenzi huo mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Tamimu Kambona, amekuwa akisimamia miradi hiyo kwa umakini kubwa.

Mafanikio hayo yaliweza kufanya ajenga maboma manne ya madarasa kati ya matatu aliyotakiwa kujenga na Serikali yakiwa na kiwango kinachostahili.

Maeneo yaliyofanikiwa kujengwa majengo hayo ni pamoja na shule ya Sekondari Engusero iliyopo kata ya Engusero iliyopatiwa mil 215 kuongeza majengo ili iweze kupokea kidato cha tano.

Kuwa pamoja na kujengwa maboma pia mabweni mawili ya wavulana na wasichana yamejengwa na kuelekezwa yaitwe Magufuli la kiume na Samia la Wasichana.

Hali hiyo imewapa wananchi matumaini makubwa kuwa mkurugenzi huyo amekuwa msaada mkubwa kwao na ambaye ameonyesha nia njema kuwa mfano kwa wenzake hapa nchini.

Kambona aliteuliwa na Rais John Pombe Magufuli, kuwa mkurugenzi wa halmashauri miezi 21 iliyopita  akitokea Mtwara kama afisa elimu wa Wilaya.

Awali wilaya ya Kiteto ilionekana kama eneo la wapiga dili katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, hali iliyofanya baadhi ya wananchi kutoaminiana nyakati zote.

Mkurugenzi Tamimu Kambona alianza kutekeleza miradi ya ujenzi vijijini na kuonyesha matunda ambapo Serikali kwa kuona hayo iliongeza fedha zaidi katika miradi wilayani humo.

Miradi bora iliyotajwa ni ujenzi wa nyumba moja ya walimu inayotumiwa na familia sita iliyoko kata ya Sunya ya thamani ya mil 150, madarasa nane katika vijiji vya Kijungu na Sunya pamoja na matundu 24 ya vyoo katika vijiji hivyo.

Miradi mingine ni madarasa manne kati ya matatu yaliyotakiwa kujengwa shule ya msingi kazingumu na Twanga iliyopo kata ya Namelock, jengo la zahanati ya Matui ambapo lengo ni kubadilishwa kuwa kituo cha afya.

Miradi hiyo imempa sifa mkurugenzi huyo baada ya kuisimamia kikamilifu na kutoa matunda, hali iliyofanya kila anayefika kuridhika na ujenzi huo kuwa na kiwango

Hata hivyo imeelezwa kuwa kila viongozi wanaofanya vizuri wilayani humo hawakai muda mrefu hivyo hofu imetandwa kwa wananchi kuwa kiongozi huyo anaweza kuondolewa muda na wakati wote na kupelekwa kwingine.

Hofu kwa wananchi kuhusu miradi kutekelezwa chini ya kiwango imetoweka na kwamba manunguniko kama ilivyokuwa awali yamepungua kutokana na usimamizi huo.

Mwisho.

Maoni