Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi William Lukuvi (kulia), Waziri wa Tamisemi Selemani Jafo (katikati) na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela (Kushoto) wakiteta wakiwa mpakani mwa Kiteto na Kilindi hivi karibuni..
Na, MOHAMED HAMAD
SERIKALI imesema, kwa mara ya kwanza itaanza kuweka mipaka inayotambulika Duniani kwa kutumia alama za namba na nukta, sio alama za kutumia milima, miti, mito na mabonde.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, aliyasema hayo jana mpakani mwa Wilaya ya Kiteto na Kilindi, wakati akitoa kauli ya Serikali kuhusu mpaka.
“Upimaji wetu wa mipaka huwa tunatumia alama..utasikia nenda kaweke kwenye mlima flani, mto flani, bonde flani, lakini wananchi wamekuwa wakipata taabu kwasasabu mito na milima huwa inahama na kwisha.
“Kwa mara ya kwanza tumeamua mpaka huu nitakao utangaza kwa kushirikiana na viongozi wenu wa vijiji, wilaya na Mkoa, tuweka alama zenye nukta zinazosomeka na mtafsiri yoyote Duniani kwa vipimo vya Kimataifa, bila kutumia alama za vitu”
Alisema Serikali itaanza na mpaka wa Wilaya ya Kiteto na Kilindi uliokuwa na mgogoro wa muda mrefu kwa kuweka GN mpya ambayo kila Kijiji kitapata nakala yake.
Uamuzi wa Waziri Lukuvi umetokana na maagizo ya Waziri Mkuu aliyotoa kutaka kuhakiki upya mpaka katika wilaya hizo kwa kutumia tangazo la Serikali namba 65 la mwaka 1961,
“Tumegundua vijiji vya Pagwi, Chamtui, na Makeleni vilivyokuwa Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga vinaonekana eneo la Kiteto, japo vinaitika Wilaya ya Kilindi.
“Uamuzi wa Waziri Mkuu na Serikali, kwa kuwa nchi hii ni moja, GN itarekebishwa ili eneo hili libaki kuwa katika Wilaya ya Kilindi kwa sababu bado linaitika Kilindi”
Alisema eneo lililosababisha mauaji lenye zaidi ya ekari elfu 15 ambalo lilihodhiwa na Wilaya ya Kiteto kinyume, baada ya kupitiwa mpaka upya kuanzia Kijiji cha Lengatei, Bonde la Mtambalo, Lembapuli, Lolela, Sosikito (Gitu).
Inaonyesha eneo lenye ekari 7, 664 liko Wilaya ya Kiteto, hekta 3709.56 ziko Wilaya ya Kilindi ambapo bonde hili ndilo lililokuwa na ugomvi mkubwa, alisema Lukuvi
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela, alisema maamuzi hayo ni salama, shirikishi ambayo yatafanya wananchi waishi kwa amani, huku Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akisema maamuzi hayo yatafikishwa kwa wananchi ili yatekelezwe kama walivyopewa maagizo.
“Kuna watu wanamiliki silaha kinyume cha sheria sio Tanga tu hata Manyara wapo, na wamekuwa wakitumia mgogoro huu kumiziza azima yao ya kuuwa wenzao, kwa upande wa Manyara nimeagiza RPC waanze kusalimisha silaha zao”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Henry Shekifu, alisema mgogoro huo uliweka chama rehani na kuipongeza Serikali kuharakisha kuutatua kwani ulifanya wananchi kukose imani na Serikali yao.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kiteto (CCM) Emmanuel Papian kwa niaba ya wananchi wake alisema, ameridhia maamuzi yaliyofanywa na serikali kupitia wataalamu na kuwataka wananchi kuwa na imani na Serikali yao.
Waziri wa Ardhi aliambatana na Waziri wanchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo, ambaye alisema ujio wao ni kusikiliza kilio cha wananchi na kutekeleza agizo la waziri Mkuu Majaliwa Kasimu Majaliwa aliyetaka wananchi kuishi kwa amani ambapo alifika hapo mwaka 2017.
Mwisho.
Maoni
Chapisha Maoni