Wadau wa Kilimo Kiteto Wapatiwa Elimu Kuhusu Kiwavijeshi Vamizi
Wadau wa kilimo wilayani Kiteto wamepata mafunzo kuhusu kisumbufu kipya cha mimea ya mahindi kinachofahamika kwa jina la Kiwavijeshi vamizi (Fall Army Worm)
Mafunzo haya yamefanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto, ambapo washiriki ni wadau wa kilimo kutoka katika makundi mbalimbali
Wamo wakulima, wauzaji wa pembejeo za kilimo, maafisa ugani, waheshimiwa madiwani, viongozi wa dini na mheshimiwa mkuu wa wilaya ambaye amewakilishwa na kaimu katibu tawala (W) ndugu Musa Waziri.
lengo la mafunzo hayo ni kujenga uelewa wa pamoja kwa wakulima dhidi ya kiwavi jeshi vamizi.
Wataalamu wa kilimo kutoka wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani ( FAO) waliwasilisha mada tatu ambazo ni utambuzi , uchunguzi na ufuatiliaji pamoja na udhibiti wa viwavijeshi vamizi.
Akiwasilisha mada ya kwanza ambayo ni utambuzi , Afisa kilimo ndugu Sergea Mutahiwa ameelekeza kuhusu namna ya kumtambua kiwavijeshi vamizi ,mzunguko wa maisha yake, tabia zake,muonekano wake.
Pia ameeleza kuhusu hali ya viwavi jeshi nchini, ushirikishwaji wadau, usambazaji wa machapisho, ushiriki wa vyombo vya habari na mtazamo wa jamii kuhusu viwavijeshi vamizi .
Akizungumzia mtazamo wa jamii, ndugu Mutahiwa amesema kwamba kwa sababu ya uelewa mdogo wa viuatilifu vinavyopendekezwa na jinsi ya kuvitumia,
Wakulima wameendelea kutumia viatilifu vingi vya aina mbalimbali, na katika maeneo mengine wakulima hutumia dozi kubwa kutokana na mashambulizi kujirudia .
Mutahiwa amesisitiza kwamba matumizi yasiyo sahihi ya viatilifu yanaweza kusababisha kuua wadudu wasiolengwa na kudhuru afya za binadamu ,vilevile kusababisha usugu kwa visumbufu vya mimea.
Aidha ameelekeza viatilifu vinavyoshauriwa na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu (TPRI) sambamba na hayo ameeleza hatua za baadae ambazo serikali kupitia wizara ya kilimo inatarajia kuzichukua ili kudhibiti kisumbufu hicho.
Mada ya pili ni ukaguzi na ufuatiliaji, mada hii imetolewa na bibi Grace David ambapo ameelekeza jinsi ya kufuatilia ukuaji wa mimea shambani, kwamba mimea inatakiwa kufuatiliwa katika ukuaji wake
Ufuatiliaji utawezesha kubaini uwepo na mwenendo wa visumbufu vya mimea katika eneo husika.
Vilevile ameelekeza namna ya kufanya ukaguzi, kwamba ukaguzi ufanyike zigizaga, usifuate mstari ili kuwakilisha shamba zima na usichukue zaidi ya dakika 15 .
Aidha Grace David amesisitiza kwamba ukaguzi ni muhimu ili kubaini uwepo na kiasi cha viwavijeshi vamizi, na kufanya tathmini ya madhara ili kuweza kujua njia sahihi ya kufanya udhibiti.
Kadhalika ameelekeza jinsi ya kutumia mtego maalum wenye harufu kwa ajili ya kukamata viwavijeshi vamizi.
Mada ya tatu ni udhibiti wa viwavi jeshi vamizi,mada hii imetolewa na ndugu Ayubu Nchimbi , ambapo ameelekeza kwamba udhibiti wa kiwavijeshi vamizi unaanza na utambuzi,
Ilielezwa kuwa lazima kumtambua kisumbufu,mzunguko wa maisha yake , dalili za mashambulizi, na kiasi gani mashambulizi yamefanyika.
Na kwamba dalili za mashambulizi ndizo zitakazomuongoza mkulima kujua kiasi cha mashambulizi, na njia atakazotumia ili kudhibiti kisumbufu.
Vilevile Nchimbi amesema kwamba udhibiti sahihi wa viwavijeshi vamizi katika ukuaji wa mimea ya mahindi unategemea na muda wa utambuzi wa mashambulizi ya mdudu kupitia ufuatiliaji na ukaguzi wa mimea shambani.
Ndugu Nchimbi ameelekeza kuhusu hatua za ukuaji wa mahindi, amesema kwamba ukuaji wa mahindi uko katika sehemu mbili; ya kwanza ni kujiimarisha kwa mmea, na ya pili ni uzaaji wa mmea.
Na kwamba ufuatiliaji ni muhimu ili kuweza kudhibiti visumbufu mapema kabla mashambulizi hayajawa makubwa.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Kiteto kaimu katibu tawala wa wilaya ndugu Musa Waziri amewataka washiriki wa semina hiyo kupeleka elimu waliyoipata katika maeneo wanayoishi.
“Mkienda kukaa kimya bila kuelimisha wengine, hiki kilichofanyika leo kitakuwa hakina maana, na mtakuwa hamkuitendea haki wizara ya kilimo pamoja na hawa wataalamu wake waliofanya kazi kubwa ya kutupatia elimu hii.
Kila mmoja aliyeshiriki semina hii ahakikishe anatoa elimu hii kwa watu zaidi ya kumi”.
Aidha Waziri amesema kwamba, kwa kuwa mkuu wa wilaya huwa anafanya mikutano mingi vijijini kila watakapokuwa katika mkutano, atahakikisha kwamba anatoa elimu ambayo ameipata katika semina hiyo.
Naye afisa Kilimo wa wilaya ndugu Robert Urassa amewashukuru washiriki wa semina kwa kuhudhuria na amewaomba ushirikiano, ili kwa pamoja waweze kuwaelimisha wakulima kama ambavyo wamepata elimu katika semina hiyo.
Katika hatua nyingine diwani wa kata ya Bwagamoyo mheshimiwa Yahya Masumbuko amesema kwamba semina hiyo imewajengea uelewa wa kutosha kuhusu kiwavijeshi vamizi.Sambamba na kauli hiyo Mhe.
Masumbuko ametoa rai kwa wizara ya Kilimo kwamba semina hizo zisiishie tu katika ngazi ya wilaya,bali zifike hadi vijijini kwani ndiko waliko wakulima wengi zaidi.
Semina hiyo imehitimishwa kwa washiriki pamoja na wawezeshaji kwenda katika shamba lililopo jirani na ofisi za TRA Kiteto ambapo wameweza kujifunza kwa vitendo jinsi ambavyo kiwavijeshi vamizi anavyofanya mashambulizi katika mimea ya mahindi, na kumuona kiwavijeshi vamizi katika hatua zote kama ambavyo wameelekezwa katika semina
Wataalamu wametoa maelezo ya kina kuhusiana na kiwavi huyo,pamoja na kujibu maswali yote ambayo yaliyokuwa yakiulizwa na washiriki ambao wamekuwa na shauku kubwa ya kufahamu zaidi baada ya kujengewa uelewa.
Maoni
Chapisha Maoni